Kufunga masiku kumi ya Dhul-Hijjah Bid´ah?


Swali: Ni yapi maoni yako kwa mwenye kusema kwamba kufunga masiku kumi ya Dhul-Hijjah ni Bid´ah?

Jibu: Huyu ni mjinga afunzwe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesisitiza mtu kufanya matendo mema ndani yake. Swawm inaingia katika matendo mema. Dalili ya hilo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakuna masiku yoyote ambayo matendo mema yanapendwa zaidi na Allaah kama masiku haya kumi.” Maswahabah wakasema: ”Hata Jihaad katika njia ya Allaah?” Akasema: ”Hata Jihaad katika njia ya Allaah. Isipokuwa tu mtu ambaye ametoka na nafsi yake, mali yake na asirudi na chochote katika hayo.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh” yake.

Ingawa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hafungi masiku haya imepokelewa kutoka kwake ya kwamba aliyafunga kama ambavyo imepokelewa vilevile kwamba hakuyafunga. Kinachozingatiwa zaidi ni yaliyosimuliwa. Maneno yana nguvu zaidi kuliko kitendo. Kukikusanyika maneno na kitendo basi Sunnah hiyo inakuwa na nguvu zaidi. Maneno yanazingatiwa kivyake, matendo yanazingatiwa kivyake na kukubali kwake kunazingatiwa kivyake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema neno, akalifanya au akalikubali yote haya yanahesabika ni Sunnah. Lakini hata hivyo maneno ndio yanayozingatiwa kuwa na nguvu zaidi, halafu kunafuata kitendo kisha kunafuata kulikubali kwake jambo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna masiku yoyote ambayo matendo mema yanapendwa zaidi na Allaah kama masiku haya.”

Kwa hivyo mtu akifunga au akatoa swadaqah basi yuko katika kheri kubwa. Vivyo hivyo imewekwa katika Shari´ah kusema ”Allaahu Akbar”, ”Alhamdulillaah” na ”Laa ilaaha illa Allaah” kwa wingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna masiku ambayo ni makubwa mbele ya Allaah na matendo yanapendwa zaidi Kwake kama masiku haya kumi. Kwa hivyo kithirisheni ndani yake Tahliyl, Takbiyr na Tahmiyd.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.binbaz.org.sa/fatawa/627
  • Imechapishwa: 22/08/2017