Kufanyakazi kwenye gazeti linaloeneza mapicha ya wanawake


Swali: Ni ipi hukumu ya kuanzisha gazeti ambalo ndani yake kuna wanawake waliovaa vibaya na isitoshe kwa njia ya kuvutia na vilevile linatilia umuhimu khabari za waigizaji wanaume na wanawake? Ni ipi hukumu ya ambaye anafanya kazi katika gazeti hili, akasaidia kulieneza na yule mwenye kulinunua?

Jibu: Haijuzu kutoa gazeti ambalo ndani yake mna kueneza picha za wanawake au linaita katika uzinzi, machafu, liwati, kunywa pombe na mfano wa hayo katika mambo yanayoita katika batili na kuyasaidia. Haijuzu kufanya kazi katika gazeti hili si kwa kuandika wala kwa kueneza kutokana na kule kusaidiana katika madhambi na uadui vinavyopatikana ndani yake. Vilevile na kueneza ufisadi katika ardhi na mwito wa kuiharibu jamii na kueneza machafu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema katika Kitabu Chake kinachoweka mambo wazi:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Shirikianeni katika wema na uchaji Allaah na wala msishirikiane katika dhambi na uadui.” (05:02)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuita katika uongofu basi ana ujira mfano wa yule atakayemfuata; hakuna chochote kitachopungua katika ujira wao, na yule mwenye kuita katika upotevu ana basi madhambi mfano wa yule atakayemfuata; hakuna chochote kitachopungua katika madhambi yao.”[1]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema vilevile:

“Kuna watu aina mbili wa Motoni sijawaona; wanaume walio na bakora kama mkia wa ng´ombe ambazo wanawapiga kwazo watu, na wanawake waliovaa vibaya, uchi, Maaylaat na Mumiylaat. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatonusa harufu yake. Harufu yake inapatikana umbali wa kadhaa na kadhaa.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

[1] Muslim (2674), at-Tirmidhiy (2674), Abu Daawuud (4609) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/209)
  • Imechapishwa: 13/08/2017