Kufanya matabano kunapingana na kumtegemea Allaah?

Swali: Kufanya matabano kunapingana na kumtegemea Allaah?

Jibu: Kumtegemea Allaah – التوكل – ni mtu kuwa na mategemezi ya kikweli kwa Allaah (´Azza wa Jall) katika kuleta manufaa na kuzuia madhara pamoja na kufanya sababu ambazo Allaah ameamrisha. Utegemeaji sio kumtegemea Allaah pasi na kufanya sababu. Kumtegemea Allaah pasi na kufanya sababu ni kumtukana Allaah (´Azza wa Jall) na katika hekima Yake (Tabaarak wa Ta´ala). Kwa sababu Allaah amefungamanisha matokeo pamoja na sababu zake. Hapa kuna swali: ni mtu ganiu mwenye kumtegemea Allaah zaidi? Ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Je, alikuwa akifanya sababu za kujinga kwazo na madhara? Ndio. Pindi alipokuwa anatoka kwenda vitani alikuwa akivaa nguo za kivita ili kujilinda na mishale. Kuna vita moja ambapo alivaa nguo za ngao. Yote hayo kwa ajili ya kujiandaa na kile kinachoweza kutokea. Kufanya sababu hakupingani na kumtegemea Allaah. Hapa ni pale ambapo mtu ataamini kuwa sababu hizi alizofanya ni sababu tu na wala hazina taathira yoyote isipokuwa kwa idhini ya Allaah (Ta´ala).

Kujengea juu ya hili mtu kujisomea mwenyewe na akawasomea ndugu zake ambao ni wagonjwa hakupingani na kumtegemea Allaah. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikuwa akijisomea mwenyewe “al-Ikhlaasw”, “an-Naas” na “al-Falaq”. Imethibiti vilevile ya kwamba alikuwa akiwasomea Maswahabah wake wanapogonjweka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (01/106)
  • Imechapishwa: 10/06/2017