Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Liharakisheni jeneza. Akiwa mwema, basi ni kheri mnayomtangulizia, na akiwa kinyume na hivo, basi hiyo ni shari mnayoiondoa kutoka kwenye shingo zenu.”[1]

Hadiyth inahimiza kuharakisha kumwandaa maiti kuanzia kule kumuosha, kumvika sanda, kumbeba, kumzika na yale yote yanayohusiana na kumwandaa. Kwa ajili hiyo ndio maana ikawa mambo haya ni katika faradhi kwa baadhi ya watu. Uharakishaji unavuliwa pale tu ambapo ikiwa kuna manufaa makubwa katika kule kumchelewesha. Kwa mfano mtu amefariki ghafla na hivyo akacheleweshwa ili kuhakikishwe sababu iliyompelekea kufa. Vivyo hivyo ikawa inataka kuongezwa ile idadi ya wenye kumswalia au wahudhurie wale ambao wana haki juu yake ambao ni ndugu na mfano wake.

Ikiwa haya yameamrishwa katika jambo la kumwandaa, basi ni jambo litalokuwa na haki zaidi kuharakisha kutakasa dhimma yake ambayo ni yale madeni na haki zinazomuwajibikia; kwani hakika ana haja kubwa ya mambo hayo.

[1] al-Bukhaariy (1315) na Muslim (944).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bahjat-ul-Abraar, uk. 97
  • Imechapishwa: 28/02/2021