Kufanya adabu kwa wazazi na kutowanyanyulia sauti

Swali: Wakati baba yangu anapokuja kuniomba kitu na mimi niko nafanya kazi au nakuwa katika wakati mgumu wakati mwingine naweza kuwanyanyulia sauti. Je, kitendo hichi ni haramu?

Jibu: Hapana shaka kwamba aliyoyafanya ni kwa sababu ya ghadhabu na dhiki ndani ya nafsi. Kinachotakikana kwa mtu ni yeye kuimiliki nafsi yake wakati wa ghadhabu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna mtu alimuuliza kwa kusema: “Niusie.” Akasema: “Usikasirike.” Akakariri kutaka kunasihiwa, akamwambia: “Usikasirike.” Kinachotakiwa ni mtu kuimiliki nafsi yake wakati wa hasira na amtake Allaah kinga dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa anapomuhisi ili aweze kuongoka. Akiweza kuimiliki nafsi yake kwa kutowanyanyulia sauti basi haitofaa kwake kuwanyanyulia sauti. Amesema (Ta´ala):

إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا

“Ikiwa mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie ´Ah` na wala usiwakemee na waambie maneno ya heshima.”[1]

Ni jambo linalojulikana kwamba wazazi wawili wanapokuwa watuwazima hufanya mambo yanayomtia mtu dhiki, kumtia uzito na kumkasirisha. Pamoja na haya Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا

“Basi usiwaambie ´Ah` na wala usiwakemee na waambie maneno ya heshima.”

Ni wajibu kwake kufanya adabu pamoja na wazazi wake wawili, kuimiliki nafsi yake wakati wa hasira na kutofanya mambo ya kuwakemea na kuwakaripia.

[1] 17:23

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (13) http://binothaimeen.net/content/6777
  • Imechapishwa: 06/02/2021