Kuchukua malipo kwa kufunza Qur-aan na kufunza elimu

Swali: Ni ipi hukumu ya kuchukua malipo kwa ajili ya kuhifadhisha Qur-aan tukufu? Sisi tuko na imamu katika kijiji chetu ambaye anapokea malipo kwa kuwahifadhisha watoto Qur-aan.

Jibu: Hakuna neno kuchukua malipo kwa kufunza Qur-aan na kufunza elimu. Kwa sababu watu wako na haja ya mafunzo. Jengine ni kwamba jambo hilo linaweza kuwa zito kwa mwalimu na likamuharibia programu zake za kuchuma [riziki]. Akichukua malipo ya kufunza Qur-aan na kufunza elimu maoni yenye nguvu ni kwamba hakuna ubaya kufanya hivo. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba kuna kundi la Maswahabah walifikia kwa baadhi ya mabedui ambapo mkuu wao akagonjweka na kwamba walijaribu kumtibu kwa kila njia lakini haikufua dafu na wakawaomba wawafanyie matabano. Mmoja katika Maswahabah akamsomea al-Faatihah ambapo Allaah akamponya. Kabla ya kufanya hivo walikuwa wamewashurutishia kuwapa kondoo. Maswahabah wakawatimiza kwa sharti hiyo. Wakajizuia kuigawanya mpaka kwanza wamuulize Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akawaambia kuwa wamefanya jambo zuri na yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaomba fungu lake. Hadiyth hiyo ameipokea al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh” yake. Hakuwakemea kitendo hicho na akasema:

”Hakika kitu chenye haki zaidi ya kukichukulia malipo ni Kitabu cha Allaah.”

Hii pia ameipokea al-Bukhaariy.

Hii ni dalili inayojulisha kuwa hapana ubaya kuchukua malipo kwa kufunza kama ilivofaa kuchukua malipo juu ya kufanya matabano.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/1291/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D8%A7%D8%AE%D8%B0-%D8%A7%D9%84%D8%A7%D8%AC%D8%B1%D8%A9-%D8%B9%D9%84%D9%89-%D8%AA%D8%AD%D9%81%D9%8A%D8%B8-%D8%A7%D9%84%D9%82%D8%B1%D8%A7%D9%86-%D8%A7%D9%84%D9%83%D8%B1%D9%8A%D9%85
  • Imechapishwa: 28/03/2020