Kuchukua malipo juu ya kuwafanyia watu matabano

Swali: Tunasikia namna ambavo baadhi ya wenye kutibu kwa Qur-aan ambao  wanasoma Qur-aan na du´aa zilizowekwa katika Shari´ah juu ya maji au mafuta masafi kwa ajili ya kutibu uchawi, kijicho na mguso wa ki-shaytwaan. Wanachukua malipo juu ya kazi hiyo. Je, kufanya hivo kunafaa kwa mujibu wa dini? Kusomea juu ya mafuta au maji kunachukua hukumu moja kama mtaalamu yeye mwenyewe akasomsomea mgonjwa?

Jibu: Hapana neno kwa mfanya matabano akachukua malipo kwa ajili ya kumsomea mgonjwa. Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na “as-Swahiyh” ya Muslim kwamba kikosi cha Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walifika katika eneo la kiarabu. Wakakataa kuwapokea. Mkuu wao akashikwa na ugonjwa ambapo wakafanya kila kitu lakini haikusaidia kitu. Wakawaendea wale Maswahabah na kuwauliza kama kuna ambaye anajua kutibu. Wakajibu: “Ndio,  lakini nyinyi mmekataa kutupokea na hivyo hatutowasomea isipokuwa kwa kutupa kondoo.” Wakakubaliana juu ya kondoo kadhaa. Mmoja katika Maswahabah akamsomea ufunguzi wa Kitabu ambapo akapona na hivyo wakawapa kile walichokubaliana. Maswahabah wakaambizana kwamba hawatofanya kitu mpaka kwanza wamtaarifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walipofika Madiynah wakamweleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yaliyotokea ambapo akawaambia:

“Mmepatia.”

Vilevile hapana neno kusoma juu ya mali na mafuta katika kumtibu mgonjwa, aliyerogwa na mwendawazimu. Lakini kumsomea mgonjwa sambamba na kumtemea cheche za mate ndio bora na kamilifu zaidi.

Abu Daawuud (Rahimahu Allaah) amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsomea Thaabit bin Qays bin Shammaas kwenye maji na akammwagia juu yake.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hapana neno kwa Ruqyah muda wa kuwa sio shirki.”

Hadiyth hii Swahiyh inajumuisha matabano kwa mgonjwa yeye mwenyewe na ndani ya maji, mafuta na vyenginevyo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (09/408)
  • Imechapishwa: 01/08/2021