Swali: Ni ipi hukumu ya kuchinja Udhhiyah ikiwa ni kwa kuchukua deni lililopangiwa muda maalum? Je, anasihi au ni lazima kwanza kwa mtu kumtaka idhini yule mwenye deni lake?

Jibu: Sioni kwamba mtu achinje ilihali yuko na deni. Isipokuwa kama amepangiwa muda maalum wa kulipa na akawa na uhakika kwamba akichukua deni hilo basi anaweza kulilipa [kabla ya muda huo kufika]. Katika hali hiyo hakuna neno akachinja. Vinginevyo achukue pesa alinazonazo na alipe deni lake. Ndugu! Deni ni kitu muhimu sana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa analetewa mtu amswalie jeneza, anaacha kumswalia. Hali ilifikia kiasi cha kwamba siku moja wapo aliletewa mmoja katika Answaar amswalia, akapiga baadhi ya hatua kisha akauliza:

“Je, yuko na deni?” Akaambiwa: “Ndio.” Akasema: “Mswalieni ndugu yenu” na yeye hakumswalia. Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) akasimama na kusema: “Dinari hizo mbili ziko juu yangu.” Ndipo akasogea mbele na kumswalia.

Isitoshe alipoulizwa kuhusu kufa shahidi katika njia ya Allaah na kama kunamfutia shahidi madhambi yake yote, akasema kwamba isipokuwa tu deni. Kufa shahidi hakufuti deni. Ndugu zangu! Deni sio kitu chepesi. Ziokoeni nafsi zenu. Msiiweke nchi katika mtihani wa uchumi katika mustakabali. Kwa sababu hawa watu ambao wanachukua madeni na wanachukulia wepesi suala la deni, watakuja kufilisika huko mbeleni. Kisha wawasababishie kufilisika wale waliochukua mikopo kwao. Kwa hiyo masuala haya ni ya khatari sana. Midhali Allaah amewafanyia wepesi waja wasifanye ´ibaadah za kimali isipokuwa wakiwa wamefunguliwa, basi mtu amhimidi na kumshukuru Allaah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (53) http://binothaimeen.net/content/1210