Kuchinja wakati wa kumalizika jengo

Swali: Huku kwetu Sudan kuna desturi ambayo pindi mtu anapoanza kujenga nyumba basi anachinja kichinjwa wakati jengo linapofika katikati. Wakati mwingine anachelewesha kichinjwa hichi mpaka jengo limalizike na akaribie kuishi ndani ya nyumba. Anawaalika kwa ajili ya kichinjwa hichi ndugu na majirani. Ni yepi maoni yako juu ya kitendo hichi? Je, kuna kitendo kilichowekwa katika Shari´ah kinachopendekezwa kufanywa kabla ya kuishi ndani ya nyumba hii?

Jibu: Kitendo hichi kinahitajia upambanuzi. Ikiwa malengo ya kichinjwa hiki ni kujilinda kutokamana na majini, malengo mengine amekusudia mwenye nyumba hii kwamba kupitia kichinjwa hichi mtu atafikia jambo fulani na fulani kama vile kusalimika yeye na kusalimika kwa jengo lake, hili ni jambo lisilofaa na ni uzushi. Ikiwa amewachinjia majini basi ni shirki kubwa. Kwa sababu ni kumfanyia ´ibaadah mwingine asiyekuwa Allaah.

Lakini kushukuru kutokana na kile alichoneemeshwa ambacho ni kule kujaaliwa kufikia kwenye paa au wakati wa kumaliza kujenga nyumba, hivyo akawakusanya ndugu na majirani zake na akawaalika katika chakula hichi, kufanya hivo hakuna neno. Jambo hili hufanywa na watu wengi kwa minajili ya kumshukuru Allaah kwa kule kuwajaalia kujenga jengo na kuishi ndani yake badala ya kupanga. Mfano wa jambo hilo ni yale yanayofanywa na baadhi ya watu wakati wanapofika kutoka safarini basi huwaalika ndugu na majirani zake kwa minajili ya kumshukuru Allaah juu ya usalama. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapofika kutoka safarini basi huchinja ngamia na akawaalika watu kwa ajili ya hilo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/355)
  • Imechapishwa: 14/02/2021