Kucheza na kushangilia wakati jua linapopatwa

Swali: Umetubainishia Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati jua linapatwa. Unawanasihi nini watu, mbali na nchi hii, ambao wanapiga dufu na wanachinja vichinjwa pindi jua linapopatwa na wanasema kuwa ni karama kwa ajili ya Allaah. Nyama hiyo wanawagawia watu. Kwa masikitiko makubwa hivi ndivyo wanavyoamini wengi wao na yanapatikana katika miji ya Kiislamu. Mkanda huu utawafikia endapo Allaah atataka.

Jibu: Nasaha zangu kwanza naanza kwa wanachuoni. Ni wajibu kwao kuwabainishia watu yale Allaah aliyowabebesha. Kwa sababu swalah ya kupatwa kwa jua sababu yake ni Allaah (´Azza wa Jall) kutaka kuwaogopesha waja Wake, kwamba inaswaliwa kwa sifa iliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ukhurafi na vitakaro hivi ni mambo yasiyokuwa na msingi. Vipi watu wataweza kuthubutu kwenda na kupiga dufu na wakacheza kwenye masoko ilihali Allaah (´Azza wa Jall) amefanya hivo kwa sababu ya kutaka kuogopesha? Uwajibu wa kwanza unawaendea wanachuoni.

Ama kuhusu watu wa kawaida ni wajibu kwao kukomeka na jambo hili, kuelekea misikitini na kutekeleza swalah ya kupatwa kwa jua kama alivyoitekeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/858
  • Imechapishwa: 19/06/2018