Kuchelewesha au kukusanya swalah kwa ajili ya kazi au masomo


Swali 11: Mimi ni mwanafunzi ninayesoma sekondari. Nidhamu za masomo zinakuwa ifuatavyo: Siku tatu za wiki ya kwanza masomo yanakuwa saa 12.30 adhuhuri. Siku tatu zengine za wiki yanakuwa saa 08.00 asubuhi. Kwa ajili hiyo napata uzito mkubwa wa kutekeleza swalah ya ´Aswr. Nikiikusanya pamoja na Dhuhr basi siku zote nachelewa. Nikichelewa hawaniruhusu kuingia pamoja na kuzingatia ya kwamba nafika nyumbani saa 05.00 alasiri. Je, inajuzu kwangu kuswali swaah ya ´Aswr saa 05.00? Je, inajuzu kuikusanya pamoja na swalah ya Maghrib?

Jibu: Ni wajibu kwako kuswali swalah zote kwa nyakati zake ijapokuwa itakuwa masomoni. Haifai kwako kuchelewesha kiasi kwamba ukaitoa nje ya wakati wake. Hivyo unatakiwa kuswali Dhuhr kwa wakati wake hata kama utakuwa kazini kwako pamoja na ndugu zako. Ukiwa uko na ndugu zako wazuri basi  swali wewe pamoja nao. Vivyo hivyo ´Aswr unatakiwa kuiswali kwa wakati wake. Haifai kwako kuichelewesha. Ikiwa wale ulio pamoja nao wanakuzuia kuswali, basi iswali baada ya kumaliza kazi midhali wakati wake bado umebaki na jua halijakuwa manjano. Katika hali hiyo unaweza kuchelewesha. Lakini ikiwa unatoka baada ya kuwa jua kuanza kuwa manjano, haifai kwako kuichelewesha. Ni lazima kwako kuswali kwa wakati. Usiwatii katika hayo. Usiwatii viongozi wako juu ya hayo hata kama kazi au masomo yataharibika. Ni wajibu kwako kuswali swalah kwa wakati wake ijapokuwa hayo yatapelekea kuacha masomo kabisa.

Ama ikiwa una uwezo wa kuswali Dhuhr kabla ya muda wake kutoka, kisha ukaswali ´Aswr kwa wakati wake baada ya masomo – kwa sababu unatoka na bado kunakuwa wakati wa kuiswali – katika hali hiyo hakuna neno. Lakini haifai kwako kuichelewesha ´Aswr mpaka jua likawa na manjano. Haifai kwako kutanguliza Dhuhr kabla ya wakati wake. Haifai kwako kuzikusanya hizo mbili. Bali unachotakiwa ni kuswali kila swalah kwa wakati wake. Hapa si pahala pa kukusanya kwa sababu ujumuishaji huu sio kwa sababu ya maradhi wala safari. Kwa sababu masomo ndio yameshughulisha. Masomo hayastahiki kuwa ni udhuru wa kukusanya. Unachotakiwa ni wewe kuswali kila swalah kwa wakati wake. Ikiwa hawakukuwezesha juu ya hilo na wakakukataza basi hakuna haja ya kazi hii. Katika hali hiyo itakulazimu kuacha kazi hiyo kwa ajili ya kuhifadhi na kupupia kuisalimisha dini yako.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziy bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Nuur ´alaad-Darb http://www.alifta.net/Fatawa/fatawaChapters.aspx?languagename=ar&View=Page&PageID=1240&PageNo=1&BookID=5
  • Imechapishwa: 15/03/2018