1Malaika wale wawili wakafika Sodoma wakati wa jioni, naye Luutw alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Wakati alipowaona, aliondoka kwenda kuwalaki na kuwasujudia hadi chini. 2Akasema: “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.” Wakamjibu: “La hasha, tutalala hapa nje uwanjani.”… 4Kabla hawajaenda kulala, watu wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba. 5Wakamwita Luutw wakisema: “Wako wapi wale watu ambao walikuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuweze kuwalawiti.” 6Luutw akatoka nje kuonana nao, akaufunga mlango nyuma yake 7akasema: “La hasha, rafiki zangu. Msifanye jambo hili ovu. 8Tazama, ninao binti wawili ambao kamwe hawajakutana kimwili na mwanaume. Acha niwatoe nje kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote watu hawa, kwa sababu wako kwenye ulinzi chini ya dari langu.” 9Wakamjibu: “Tuondokee mbali.” Wakaendelea kusema: “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Luutw na kusonga mbele ili kuvunja mlango. 10Lakini watu wale waliokuwa ndani wakanyoosha mkono wakamvuta Luutw ndani ya nyumba na kufunga mlango. 11Kisha wakawapiga kwa upofu wale watu waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango. 12Wale watu wawili wakamwambia Luutw: “Una mtu mwingine yeyote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa 13kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa Bwana dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.” 14Kwa hiyo Luutw alitoka ili kuzungumza na wakwe zake waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia: “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa Bwana yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania.

15 Kunako mapambazuko Malaika wakamhimiza Luutw, wakamwambia: “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.” 16 Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa Bwana alikuwa na huruma kwao. 17Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia: “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!” 18Lakini Luutw akawajibu: “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! 19Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa. 20Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.” 21Akamwambia: “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. 22Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.)

23Wakati Luutw alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. 24NdipO Bwana akanyesha moto wa kiberiti uliotoka mbinguni kwa Bwana juu ya Sodoma na Gomora. 25Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote waliokuwa wanaishi katika miji, hata pia mimea yote katika nchi. 26Lakini mke wa Luutw akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi. 27Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Ibraahiym akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za Bwana. 28Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka kwenye nchi, kama moshi utokao kwenye tanuru. 29Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare alimkumbuka Ibraahiym, akamtoa Luutw kutoka kwenye lile janga lililoharibu miji ile ambamo Luutw alikuwa ameishi.

  • Mhusika: Biblia
  • Mfasiri: https://www.bible.com
  • Marejeo: Mwanzo 19:01-29
  • Imechapishwa: 21/11/2018