Kuacha swalah ni dhambi kubwa zaidi kuliko uzinzi na wizi

Swali: Je, swalah ya sunna ya Fajr, Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa zinatosheleza kutokamana na kulipa swalah kwa sababu mimi sikuwa mwenye kuswali kwa miaka mingi? Au ni lazima kwa mtu kuzilipa swalah hizi za faradhi ambazo shaytwaan amemkengeusha nazo?

Jibu: Mwenye kuacha swalah za faradhi kwa makusudi, uvivu na kwa kuzembea basi amefanya dhambi kubwa zaidi kuliko zinaa, wizi na dhambi nyenginezo kubwa. Isitoshe kwa kufanya hivo anakufuru kufuru kubwa kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh).

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Pia kutokana na Hadiyth nyenginezo zilizo na maana kama hiyo.

Akiacha swalah kwa kupinga uwajibu wake basi anakufuru ukafiri mkubwa kwa maafikiano ya waislamu. Ni lazima kwa ambaye ameacha hali ya kupinga uwajibu wake, uvivu na kuzembea akimbilie kutubu kwa Allaah (Subhaanah) kutokana na hilo. Anafanya hivo kwa kujutia yale yaliyotangulia, maazimio ya kweli asirudi kuiacha. Sambamba na hilo aichunge hali ya kumwogopa Allaah, kumtukuza na kutekeleza haki Yake. Mwenye kutubu tawbah ya kweli basi Allaah humsamehe. Amesema (Subhaanah):

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا

“Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya kwelikweli.”[2]

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akanyooka barabara.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutubu juu ya dhambi ni kama ambaye hana dhambi.”

Haimlazimu kulipa zile swalah alizoacha. Kwa sababu tawbah ya kweli inamtosha kutokamana na hilo.

[1] 24:31

[2] 66:08

[3] 20:82

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/323)
  • Imechapishwa: 07/10/2021