Kuacha Basmalah kabla ya kutawadha kwa kusahau


Swali: Nilitawadha na sikumbuki kuwa nilisema “Bismillaah” isipokuwa baada ya kumaliza kuosha mikono miwili. Nilipokumbuka nikarudi kutawadha upya. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Jopo la wanazuoni walio wengi wameonelea kuwa wudhuu´ unasihi pasi na kusema “Bismillaah”. Wanazuoni wengine wakaonelea kuwa ni lazima kusema “Bismillaah” ikiwa mtu anajua na amekumbuka kufanya hivo. Imepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Hana wudhuu´ ambaye hakutaja jina la Allaah juu yake.”

Lakini kuhusu ambaye ataacha kufanya hivo kwa kusahau au pasi na kujua basi wudhuu´ wake ni sahihi. Haimlazimu kurudi kutawadha hata kama tutaonelea kuwa ni lazima kusema “Bismillaah”. Kwa sababu ni mwenye kupewa udhuru kutokana na ujinga na kusahau. Hoja katika hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Allaah ameitikia du´aa hii.”

Kwa hivyo inapata kufahamika kwamba unaposahau kusema “Bismillaah” mwanzoni mwa wudhuu´ kisha ukakumbuka mwishoni mwake basi unatakiwa kuileta. Hulazimiki kurudi kutawadha upya kwa sababu ni mwenye kupewa udhuru.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/100)
  • Imechapishwa: 11/08/2021