Kimsingi ni kuoa wake wengi na manufaa yanayopatikana katika hilo

Swali: Watu wengi wanapinga jambo la kuoa wake wengi na baadhi yao wanafikiria kuwa ni jambo limeharamishwa. Hii leo katika jamii kuna ujasusa unaofanywa ambao ni khatari.

Jibu: Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne.”[1]

Msingi ni kuoa wake wengi. Hilo ni kwa ajili ya manufaa kwa wanamme na wanawake. Kuoa wake wengi kunamfaa mwanamme na mwanamke. Wakati fulani pengine mke mmoja asimtoshi mwanamme. Mwanamme anaweza kuwa na matamanio yenye nguvu na hivyo mke mmoja asimtosheleze. Matokeo yake akahitajia kuoa wake wawili, watatu na wananne ili aweze kuiheshimisha nafsi yake, aweze kuteremsha macho chini na kuihifadhi tupu yake.

Vivyo hivyo wanawake wanawahitajia wanamme. Wanamme wote wakitosheka na mke mmoja, basi wanawake wengi watabaki pasi na waume. Wanawake wakiolewa wengiwengi basi wanawake watakuwa na manufaa kwa jambo hilo. Mwanamke kuolewa na mume ambaye tayari ana mke ni bora kuliko kubaki hali ya kuwa hana mume.

Tunachokusudia kusema ni kwamba kuoa wake wengi ndio Sunnah, jambo jema zaidi na lenye manufaa zaidi kwa jamii ikiwa mume ana uwezo wa kufanya hivo. Kitendo cha mwanamke kupewa nusu, theluthi au robo ya mwanamme ni bora kwake kuliko kubaki hali ya kutoolewa pasi na mwanamme yeyote.

Wanawake wanatakiwa walitambue jambo hili na watahadhari kuwa na wivu unaodhuru. Vivyo hivyo yanawahusu wale wasimamizi na walezi wao. Haitakiwi kwa mwanamke kukataa kuolewa na mume ambaye tayari yuko na mke mmoja, wawili au watatu. Allaah ndiye kamhalalishia jambo hilo. Ndani yake kuna manufaa mengi kwa wanamme na wanawake wote wawili.  Jambo hilo linazihifadhi tupu ya mwanamme na mwanamke, kushusha macho chini, kuwasaidia wanawake mafakiri na kuwasimamia na pia kuwatetea na kuwalinda kutokamana na maharibifu.

Kuoa wake wengi ndani yake kuna kheri na manufaa mengi. Lakini wanawake wengi hawalitambui hilo. Baadhi ya wasimamizi na walezi wa wanawake hawalitambui hilo. Wanatakiwa wazinduke juu ya jambo hili.

Vivyo hivyo kila kilichowekwa na Allaah katika Shari´ah ndani yake kuna manufaa makubwa. Pengine watu wasiyajue. Allaah hajaweka jambo la ukewenza isipokuwa kwa sababu ya manufaa.

Waliokuwa kabla yetu mwanamme alikuwa anaruhusiwa kukusanya wanawake tisini mpaka mia. Sulaymaan bin Daawuud (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alikuwa na wanawake tisini. Baba yake Daawuud (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na wanawake mia. Baadaye ndipo Allaah akakataza katika Shari´ah ya Muhammad kuzidisha wake wanne kwa ajili ya kuwawepesishia Ummah huu. Ndipo wakafanyiwa wake wanne peke yake. Lakini baadhi ya wanawake hawayatambui haya kama ambavo walivyo baadhi ya wasimamizi na walezi wao pia. Hawatambui manufaa haya. Ndio maana wengi wao wanachukia, wanakataa na wanapinga kuoa wake wengi.

Baadhi ya walinganizi wa batili katika vyombo vya mawasiliano wanafanya mambo ambayo yanamkimbiza mwanamke kuolewa na mwanamme ambaye tayari amekwishaoa kana kwamba kitendo hicho ni cha jinai. Hawa wanaofanya hivi ima ni wajinga juu ya amri ya Allaah au ni mafasiki na ni wenye kumwasi Allaah. Tunamuomba Allaah afya.

Kwa hivyo ni lazima kuzinduka juu ya jambo hili.  Ni lazima kwa muumini kuridhia yale yaliyowekwa na Allaah katika Shari´ah. Allaah (Subhaanah) amesema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

“Hivyo kwa sababu wao wameyachukia ambayo ameteremsha Allaah, basi akayaporomosha matendo yake.”[2]

Ni lazima kwa waumini wa kiume na wa kike kuridhia yale yaliyowekwa na Allaah katika Shari´ah, kuyapenda na kutoyachukia.

[1] 04:03

[2] 47:09

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/4318/%D9%85%D8%A7-%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%86%D8%A7%D9%81%D8%B9-%D8%A7%D9%84%D8%AA%D9%8A-%D8%AA%D8%AD%D8%B5%D9%84-%D8%A8%D8%AA%D8%B9%D8%AF%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%AC%D8%A7%D8%AA
  • Imechapishwa: 03/06/2020