Kilichopo ni sujudu ya kushukuru na sio swalah ya kushukuru

Swali: Ni ipi sifa ya swalah ya kushukuru na swalah ya Istikhaarah?

Jibu: Sijui kupokelewa chochote kuhusiana na swalah ya kushukuru. Kilichopokelewa ni sujudu ya kushukuru na swalah ya tawbah. Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa mtu pindi anapofanya dhambi basi aswali Rak´ah mbili na atubie kwa Allaah tawbah ya kweli. Hii ndio swalah ya tawbah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mja yeyote atakayefanya dhambi, kisha akajitwaharisha na kufanya vizuri twahara yake, kisha akaswali Rak´ah mbili na akatubu kwa Allaah kutokamana na dhambi hiyo, isipokuwa tawbah yake itakubaliwa.”[1]

Ameipokea Imaam Ahmad kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia Hadiyth ya Abu Bakr as-Swiddiyq.

Vivyo hivyo sujudu ina sujudu iliowekwa katika Shari´ah. Akibashiriwa kitu chenye kumfurahisha, mambo ya waislamu kufunguka, waislamu kushinda dhidi ya maadui wao au chenginecho cha kumfurahisha, basi atamsujudia Allaah hali ya kumshukuru. Kama mfano wa sujudu ya swalah. Atasema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Allaah, Aliye juu, kutokamana na mapungufu.”

na ataomba du´aa ndani ya sujudu yake, kumhimidi Allaah, kumsifu kwa kheri aliyopata. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimsujudia Allaah hali ya kumshukuru anapojiwa na kitu cha kumfurahisha. Wakati [Abu Bakr] as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) alipobashiriwa juu ya kuuawa kwa Musaylamah alimsujudia Allaah kumshukuru. Wakati ´Aliy (Radhiya Allaah ´anh) alipompata mwombozi katika wauliwaji wa Khawaarij alimsujudia Allaah akimshukuru.

Kuhusu swalah ya Istikhaarah ni kama swalah zengine pia. Ni Rak´ah mbili ambazo atasoma ndani yake al-Faatihah na chenginecho kitachomsahilikia. Baada ya kutoa salamu atanyanyua mikono yake na atamuomba ushauri kwa kusema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْتَخيرُكَ بِعِلْمِكَ وأَسْتَقْدِرُكَ بقدرَتِكَ وأَسْأَلُكَ منْ فَضْلِكَ الْعَظِيمِ فَإِنَّكَ تَقْدِرُ وَلاَ أَقْدِرُ وَتَعْلَمُ وَلاَ أَعْلَمُ وَأَنْتَ عَلاَّمُ الْغُيُوبِ اللهُمَّ إِنْ كُنتَ تَعلم أَنَّ هذَا الأَمْرَ خيرٌ لِي في دِيني وَمَعَاشي وَعاقِبة أَمْرِي وَعَاجِلِهِ وَآجِلِهِ فاقْدُرْهُ لِي وَيَسِّرْهُ لي ثمَّ بَارِكْ لي فيهِ وَإِنْ كُنْتَ تَعْلَم أَنَّ هَذا الأَمْرَ شَرٌّ لِي في دِينِي وَمَعَاشِي وَعَاقِبَةِ أَمْرِي وَعَاجِلِهِ وَآجِلِهِ فاصْرِفْهُ عَنِّي واصرفْنِي عَنْهُ واقْدُرْ لِيَ الْخَيْرَ حَيْثُ كانَ ثم رضِّنِي بهِ

“Ee Allaah! Hakika mimi ninakutaka kwa ujuzi Wako na ninakuomba uniwezeshe kwa uwezo Wako. Ninakuomba kwa fadhila Zako kubwa. Hakika Wewe unaweza na mimi siwezi. Wewe unajua na mimi sijui. Wewe ni Mjuzi wa yale yaliyofichikana. Ee Allaah! Endapo unajua kuwa jambo hili – litaje jambo lako – ni kheri kwangu katika Dini yangu, mwisho wa maisha yangu duniani na Aakhirah, basi nakuomba uniwezeshe na unisahilishie, kisha nibariki kwalo. Na endapo unajua kuwa jambo hili ni shari kwangu katika dini yangu, mwisho wa maisha yangu duniani na Aakhirah, basi nakuomba liepushe na mimi na mimi uniepushe nalo, na nipangie jambo jengine lenye kheri na mimi popote lilipo, halafu niridhishe kwalo.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Ahmad (02) na Ibn Hibbaan (623).

[2] al-Bukhaariy (1096).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/424)
  • Imechapishwa: 16/11/2019