Swali: Je, yapo mambo maalum yaliyowekwa katika Shari´ah ambayo muislamu anaipokea Ramadhaan kwayo?

Jibu: Mwezi wa Ramadhaan ndio mwezi bora katika mwaka. Allaah ameufanya kuwa maalum kwa kujaalia funga yake kuwa ni faradhi na nguzo ya nne katika zile nguzo za Uislamu na pia amewawekea Shari´ah waislamu kufunga nyusiku zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa yule mwenye kuweza kuiendea.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Na yule atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[2]

Sijui kitu maalum cha kuipokea Ramadhaan zaidi ya muislamu kuipokea kwa furaha, shangwe, kumshukuru Allaah kumfikishia Ramadhaan na kumjaalia kuwa ni miongoni mwa wale hai ambao wanashindana katika matendo mema. Hakika kufika kwa Ramadhaan ni neema kubwa kutoka kwa Allaah.

Imepokelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapongeza Maswahabah zake kwa kufika kwa Ramadhaan hali ya kubainisha fadhilah zake, yale Allaah aliyowaandalia wafungaji na wenye kusimama kuswali katika thawabu kuu. Pia imesuniwa kwa muislamu kupokea mwezi huu mtukufu kwa tawbah ya kweli na kujiandaa kuufunga na kusimama kuswali kwa nia njema na azimio ya kweli.

[1] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[2] al-Bukhaariy (1901) na Muslim (760).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (09/15)
  • Imechapishwa: 17/04/2020