Kila ambavyo mwanaume ataoa wake wengi ndio bora zaidi

Swali: Kuna jambo muhimu limekithiri katika jamii ambalo ni kuwepo kwa utasa kwa baadhi ya wanawake. Huenda hilo linatokana na maumbile yenyewe au moja katika sababu ni kutumia dawa za kuzuia mimba mwanzoni mwa ndoa. Pili kutumia dawa za kuzuia hedhi. Tatu pengine zikawa ni njama wanazotumia maadui ambazo hatuzijui. Je, mume ana haki ya kuoa mwingine kwa sababu ya kuchelewa kupata watoto kwa miaka mingi? Anampenda mke wake lakini anachelea asije kumdhulumu kwa kitu ambacho yeye mwanamke hana uhusiano nacho? Ni zipi nasaha zako? Je, unajua dawa za Kishari´ah juu ya hilo?

Jibu: Katika wakati huu au katika zama hizi kumekithiri utasa na pia kumekithiti watoto wachanga wanaozaliwa walemavu. Hilo ni kwa sababu baadhi ya wanawake – Allaah awaongoze – wanatumia dawa za kuzuia hedhi au kuzuia mimba. Matokeo yake mwanamke anaadhibiwa kwa kitendo hichi na mume pia ambaye amempa idhini ya kufanya hivo anaadhibiwa kwa hili. Kwa ajili hiyo nawashauri ndugu zangu wayaache mambo kama yalivyo kimaumbile. Kizazi kikiwa kingi basi hiyo ni katika neema za Allaah. Hilo ndilo ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitaka katika Ummah huu pale aliposema:

“Oeni wanawake wenye mapenzi na wenye kuzaa sana. Kwani hakika mimi nitajifakharisha kwa ajili yenu Mitume wengine siku ya Qiyaamah.”

Ama swali lake analouliza kama inafaa kwake kuoa mwanamke mwingine juu yake? Ndio, oa juu yake hata kama mwanamke huyo anazaa. Oa mwanamke wa pili. Ukitaka tena na wakati huohuo ukawa na uwezo wa kimali na wa kimwili basi oa wa tatu. Ukiwa na uwezo ongeza mwingine wa nne. Kila ambavyo mwanaume ataoa wanawake wengi ndio bora zaidi. Mtu akiwa na uwezo wa kimali na wa kimwili. Vilevile awe na uwezo wa kufanya uadilifu. Kwa msemo mwingine aweze kufanya uadilifu kati yao. Ama akiwa anachelea hatoweza kufanya uadilifu, akawa ni fakiri au hana uwezo, katika hali hii tunamwambia atosheke na mke mmoja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (55) http://binothaimeen.net/content/1258
  • Imechapishwa: 01/10/2019