Swali: Namshuhudisha Allaah ya kwamba mimi nakupenda kwa ajili ya Allaah. Mimi ni kijana ambaye sizidi umri wa miaka kumi na tano na mimi – Allaah akitaka – ni miongoni mwa vijana wenye msimamo wa dini. Lakini nyumbani kwetu kuna mfanyakazi wa kike ambaye ni mrembo. Je, ni sahihi nikamuona pamoja na kuzingatia ya kwamba siwezi kumtoa kwa sababu mama yangu ni mgonjwa na mama yangu pia humuhitajia. Lakini mwanamke huyu hunijia mpaka usingizini. Ni zipi nasaha zako kwangu na kwa mwanamke huyu?

Jibu: Akupenda yule ambaye umenipenda kwa ajili yake. Ndugu! Napenda kukujuzeni kwamba kupendana kwa ajili ya Allaah ni miongoni mwa mafundo yenye nguvu kabisa ya imani.

Ama kuhusu kushikamana kwake na dini basi namuomba Allaah atuthibitishe sisi na yeye juu ya haki.

Kuhusiana na mwanamke mfanyakazi huyo wa kike mimi naona kwamba anatakiwa kumkimbia kama anavyomkimbia simba. Asimzungumzishe na wala asimtazame. Afanye bidii kumrejesha na badala yake alete mfanyakazi ambaye hatokuwa na fitina kwake. Ni jambo linalotambulika kwamba mfanyakazi huyu kama ni mrembo na yeye bado ni kijana ima kijana huyu akamwita au mwanamke huyu yeye akamwita. Ni lazima shaytwaan atie kati yao wasiwasi mpaka awatumbukize katika shari.

Kwa ajili hiyo nasema ikiwa anaweza kumhudumia mama yake kama ambavo anafanya mfanyakazi huyu na asimbakize nyumbani itakuwa ni bora zaidi. Mimi naona kwamba aharakishe kumpatia mfanyakazi huyu haki yake na amrejeshe kwa familia yake na badala yake alete mfanyakazi ambaye hatofitinishwa naye. Vinginevyo jambo hili ni la khatari. Hata kama halikutokea kwa sasa litatokea huko baadaye isipokuwa akitaka Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sijaacha fitina ambayo ni yenye madhara zaidi kwa wanaume kama wanawake.”

Kwa mnasaba huu nasema kwamba ukhatari wa wafanyakazi wa kike ni mkubwa sana. Mwanzoni nilikuwa nachukulia usahali juu ya masuala ya kumleta mfanyakazi wa kike bila Mahram. Kwa msemo mwingine akimleta mwanamke huyu kisha akarudi huyu aliyemleta hakuna neno. Lakini baada ya kusikia mambo yaliyonichukiza ndipo nikaona kuwa ni lazima mfanyakazi mwanamke aje pamoja na Mahram wake na awe ni mwenye kuambatana naye mpaka siku ile ataposafiri kurudi. Tumesikia mambo ya ajabu ambayo sitaki kuyataja. Kwa sababu mambo hayo yanamuhuzunisha kila muislamu.

Ni wajibu kumcha Allaah juu ya nafsi zetu na juu ya jamii zetu. Imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakutoenea uzinzi kwa watu isipokuwa kutaenea ukame ambao haukuwahi kutokea kwa waliotangulia.”

Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na hayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (50) http://binothaimeen.net/content/1142
  • Imechapishwa: 17/06/2019