Kijana anakhofu asiwe mnafiki kwa kudhihirisha msimamo ilihali ni mpiga punyeto

Swali: Mimi ni kijana mwenye msimamo ambaye nimehifadhi sehemu kubwa ya Qur-aan. Nimepewa mtihani ambao ni kujichua sehemu ya siri. Je, ni katika unafiki kuwaonyesha watu kuwa na msimamo na kuficha dhambi hii? Ni ipi dawa ya kuacha punyeto?

Jibu: Hii haihesabiki kuwa ni unafiki. Kule mtu kujisitiri na sitara ya Allaah katika kumuasi Allaah hakuhesabiki kuwa ni unafiki. Anamcha na kumukhofu Allaah na pia anamuamini Allaah (´Azza wa Jall). Jengine ni kwamba anatambua kosa lake na anamuonea aibu Allaah (´Azza wa Jall). Huu sio unafiki.

Inatakiwa kwa mtu anapofanya dhambi asimweleze yeyote juu ya hilo. Kuna Hadiyth imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Ummah wangu wote ni wenye kusamehewa isipokuwa wale kuonyesha [madhambi] hadharani.”

Hawa ni wale wenye kufanya maasi halafu kunapopambazuka wanawaeleza watu. Huyu hayuko katika usalama. Hakuna ambaye ni mpole kwako, mwenye huruma zaidi kwako na mwenye kupenda zaidi msamaha kama Allaah. Unapofanya makosa na usimweleze yeyote basi dhambi inabaki kati yako wewe na Allaah. Hapa tatizo limekwisha. Tunamwambia ndugu huyu: jisitiri kwa sitara ya Allaah. Huku sio kufanya unafiki. Kimbilia kwa Allaah ufanye tawbah ya kweli.

Ikiwa umepewa mtihani wa janga hili basi elewa kuwa ni haramu na ni jambo lina athari mbaya inapokuja kwenye mwili na khaswa katika mustakabali wa mtu. Mtu mwenye busara anatakiwa kuifanya akili ikaamua. Mwenye busara ni yule ambaye anaifanya akili kuyashinda matamanio yake. Jiepushe na jambo hili na ujikwamue nalo. Vilevile kimbilia katika suala la kuoa mapema kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi kongamano la vijana! Yule katika nyinyi atakayeweza kuoa basi aoe. Hakika kufanya hivo kunawafanya kuyateremsha macho chini na kuzihifadhi tupu. Yule asiyeweza basi afunge.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (31) http://binothaimeen.net/content/703
  • Imechapishwa: 28/10/2017