Allaah (Ta´ala) amesema:

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

“Imeenea Kursiy Yake mbingu na ardhi.” (02:255)

´Arshi ndio kiumbe kikubwa kabisa. Kisha kiumbe kinachofuatia kwa ukubwa ni Kursiy na hiki ni kiumbe kikubwa. Kuna ambao wamenukuu na kusema kuwa Kursiy ni elimu ya Allaah. Lakini hata hivyo hii ni kauli dhaifu na kumnasibishia kauli hii Ibn ´Abbaas haikuthibiti. Elimu ya Allaah imekienea kila kitu. Kama alivosema (Ta´ala):

رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا

“Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rehema na elimu.” (40:07)

Allaah anajijua Mwenyewe, anajua yaliyoko na yasiyokuwepo. Ikiwa Kursiy katika Aayah itafasiriwa kuwa ni elimu basi ingelisemwa:

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

“Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi.”

Maana hii isingelikuwa ya sawa na khaswa ukizingatia ya kwamba Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا

“Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo.” (02:255)

bi maana havimuwii vizito. Haya ndio yanayoenda sambamba na uwezo na si elimu.

Wengine wakasema kuwa Kursiy ndio ´Arshi. Lakini hata hivyo wengi wanaonelea kuwa ni mambo mawili tofauti. Kwa hivyo kauli zinakuwa tatu.

Sahihi ni kwamba Kursiy ni kiumbe kingine mbali na ´Arshi. Kursiy ni mahala ambapo Mwingi wa  rehema (Jalla wa ´Alaa) anapoweka Miguu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/396)
  • Imechapishwa: 19/05/2020