Swali: Mwanzoni wa mwaka katika ndoa yetu nilipatwa na khasira nyingi nikamuapia mke wangu Talaka, nikamwambia: “Mama yako akiingia hapa utakuwa ni mwenye kutalikika”, na nilikuwa nimekusudia kumkataza asifanye hivyo na si Talaka. Na baada ya hapo mama yake akaingia na ndoa yetu ikaendelea mpaka sasa ni zaidi ya miaka 20 na nikazaa nae watoto na sikumuapia Talaka mara nyingne kwa kiasi cha muda wote huu. Ni ipi hukumu ya Talaka hii, imepita au hapana?

Jibu: Kauli iliyo ya sahihi ni kuwa, Talaka hii hukumu yake ni ya yamini. Kwa kuwa hukukusudia kumtaliki, bali ulikusudia kum-kataza mama yake asiingie. Talaki hii hukumu yake inakuwa ya yamini kutokana na kauli sahihi ya wanachuoni. Ni juu yako kukafiria yamini yako hata kama muda umekwishapita; kwa kulisha masikini 10 au kuwa-visha nguo, au kuachia mtumwa huru. Kama Alivyobainisha Allaah katika Kitabu Chake Kitukufu katika Suurat-ul-Maaidah. Na kila masikini mmoja utampa 1,5 kg ya tende, mchele au visivyokuwa hivyo katika vyakula (vilivyozoeleka) katika mji, watapewa masikini 10. Au kuwakatia nguo, kuwapa kanzu au kikoi na nguo ya juu. Kufanya kwako hivi yatosha. Alhamduli Allaah. Na wala Talaka itakuwa haikupita na mke atabaki kuwa ni wako. Na wala haidhuru kwa muda wote huu mrefu. Isipokuwa tu ulikosea kwa kukawia kutoa kafara kwa muda wote huu mrefu. Ama kauli inayosema kuwa Talaka inapita (katika hali kama hii), ni kauli dhaifu. Kauli iliyo ya sahihi ni kuwa haipiti, maadamu makusudio yako ilikuwa ni kumkataza na kumzuia na haikuwa kumtaliki.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 27/03/2018