1568- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kama wewe kweli ni mja wa Allaah, basi kipandishe kikoi chako.”

Ameipokea Ahmad (2/141): Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan at-Twafaawiy ametuhadithia: Ayyuub ametuhadithia, kutoka kwa Zayd bin Aslam, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Niliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikiwa nimevaa kikoi chenye kuburutaburuta. Akasema: “Ni nani huyo?” Nikasema: “Ni ´Abdullaah bin ´Umar.”  Akasema: “Kama wewe kweli ni mja wa Allaah, basi kipandishe kikoi chako.” Nikakipandisha kikoi changu mpaka nusu ya muundi. Hakuacha kuendelea kukaa kikoi chake hivo mpaka alipofariki.”

Mlolongo wa wapokezi ni Swahiyh na ni kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

Katika Hadiyth kuna dalili ya wazi kabisa yenye kuonyesha kuwa haijuzu kwa muislamu kurefusha kikoi chake kikaenda chini ya kongo mbili za miguu. Bali ni lazima kwake kukipandisha juu ya kongo mbili za miguu. Haijalishi kitu hata kama lengo lake yeye sio kiburi. Hapa kuna Radd ya wazi kwa baadhi ya wanachuoni ambao wanayarefusha majuba yao mpaka yanakaribia kugusa chini. Wanadai kwamba hawafanyi hivo kwa kiburi. Ni kwa nini basi wameiacha amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Ibn ´Umar? Je, wao mioyo yao ni misafi zaidi kushinda wa Ibn ´Umar?

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (4/95)
  • Imechapishwa: 12/05/2019