Kalima makaburini sawa na si mawaidha na kuhubiri

Swali: Inajuzu kuwawaidhi watu makaburini? Je, inajuzu kwa mmoja kuomba na wengine wakaitikia “Aamiyn”? Je, ikiwa kitendo hichi ni cha sawa basi ni ipi du´aa bora? Ikiwa ni jambo ambalo halijuzu basi nakuomba uwawekee watu wazi.

Jibu: Kuhusu kuwawaidhi watu kwa njia maalum ni sawa. Kwa mfano mtu amekaa na pembezoni mwake wako watu na akaanza kuzungumzia kuhusu kifo, yaliyo baada yake, yale anayohojiwa maiti juu ya Mola, dini na Mtume wake ni jambo zuri. Au kwa mfano amekaa karibu na kaburi na akaanza kuwanukulia watu yale yaliyosemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja ambapo alikuwa anamzika mmoja wa wasichana wake akasema:

“Hakuna kati yenu yeyote isipokuwa yameshaandikwa makazi yake Peponi na makazi yake Motoni.”

Kila kitu kimeshaandikwa. Tunamuomba Allaah atujaalie makazi yetu yawe ya Peponi. Kila kitu kimeshaandikwa. Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Basi si tuache kufanya matendo?” Kwa vile midhali kila kitu kimeshaandikwa. Akawajibu: “Tendeni! Kila mmoja ni mwenye kusahilishiwa kile aliachoandikiwa.” Mtu ambaye makazi yake ni Peponi hawezi kufanya matendo ya watu wa Motoni na mtu ambaye makazi yake ni Motoni hawezi kufanya matendo ya watu wa Peponi. Bi maana ni matendo ambayo yameandikwa ambayo yanapelekea katika makazi haya. Kalima kama hii haina neno.

Vilevile kuna siku miongoni mwa siku Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwenye makaburi ya al-Baqiy´ ambapo walikuwa wakimzika mwanaume mmoja katika Answaar. Lakini walikuwa hawajachimba mwanandani. Watu walikuwa wanasubiri mwanandani huu utimie. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakaa chini na watu wakakaa pembezoni mwake hali ya kutulia kana kwamba ndege zimeketi juu ya vichwa vyao. Hii ni heshima kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakiiheshimisha sehemu hii. Akaanza kuwaelezea yanayopitika wakati  mtu anapotaka kukata roho na yaliyo baada ya kifo. Kalima kama hii haina neno.

Ama mtu kuanza kuwahubiria watu ni jambo ambalo halina uhusiano wowote na Sunnah. Haikuthibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah walikuwa wakihubiri na kuwatolea watu mawaidha kwenye makaburi. Mawaidha na Khutbah yanafanywa wapi? Misikitini. Si makaburini. Makaburini ni sehemu ya kuazi. Lakini kukitokea mnasaba ni sawa kufanya kalima na sio Khutbah.

Kuhusu kumuombea maiti du´aa baada ya kuzika basi itambulike kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akiomba du´aa na huku watu wanaitikia “Aamiyn”. Hata siku moja! Alichokuwa akifanya baada ya kumaliza kumzika maiti anasimama karibu na maiti yule na kusema:

“Mstaghufirieni ndugu yenu na mumuombee uimara. Kwani hakika hivi sasa atahojiwa.”

Kujengea juu ya hili unatakiwa kusimama karibu na kaburi na kusema:

“Ee Allaah! Msamahe. Ee Allaah! Msamahe. Ee Allaah! Msamahe. Ee Allaah! Mthibitishe. Ee Allaah! Mthibitishe. Ee Allaah! Mthibitishe.”

Mara tatu kisha unaondoka. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapoomba basi anaomba mara tatu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (31) http://binothaimeen.net/content/709
  • Imechapishwa: 04/11/2017