Kafiri asiyeswali hazikwi kwenye makaburi ya waislamu


Swali: Hukumu ya mwenye kuacha Swalah na je anazikwa katika makaburi ya Waislamu?

Jibu: Kuhusiana na mwenye kuacha Swalah kwamba atazikwa katika makaburi ya Waislamu, wanachuoni wametofautiana kuhusiana na hukumu yake.

1) Akiacha kwa uvivu na wala hapingi uwajibu wake, anaamini kuwa Swalah ni wajibu lakini akaacha kwa uvivu na kuzembea, kuna ambao wanaona kuwa hakufuru kufuru kubwa, bali ni kufuru ndogo. Na kwamba anazikwa pamoja na Waislamu wengine, kuoshwa na kuswaliwa. Hii ni kauli maarufu kwa kundi kubwa la wanachuoni.

2) Kauli ya pili ni kuwa, anakufuru kufuru kubwa. Na hii ndio kauli iliyo ya sahihi. Kutokana na hili, hatozikwa pamoja na Waislamu, bali atatafutiwa mahali afukiwe na asiachwe juu ya ardhi. Atazikwa kama ilivyo kwa makafiri wengine. Kutokana na kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Ahadi iliopo baina yetu sisi na wao ni Swalah, atakayeiacha amekufuru.”

Na wala hakubagua yeyote, na wala hakusema ikiwa anapinga uwajibu wake (hakufuru). Na hii ni Hadiyth Swahiyh imepokea Ahmad na Ahl-us-Sunan kwa isnadi Swahiyh. Na Muslim kapokea katika Swahiyh yake, kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema:

“Baina ya mja na baina ya kufuru na Shirki ni kuacha Swalah.”

Shirki na kufuru inapokuja kwa sampuli hii inakuwa kubwa. Hii ndio kauli iliyo sahihi na yenye nguvu pamoja na kuwa kuna dalili zingine nyingi ambazo zinaonesha kuwa hata kwa mwenye kuacha Swalah kwa uvivu, hana lolote katika Uislamu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alharamain.gov.sa/index.cfm?do=cms.scholarallsubjects&schid=8177
  • Imechapishwa: 20/01/2018