Kafiri akisilimu au mtoto akabaleghe katikati ya Ramadhaan atalazimishwa kufunga siku zilizopita?

Swali: Mtu akisilimu baada ya baadhi ya masiku ya Ramadhaan alazimishwa kulipa masiku yaliyopita?

Jibu: Huyu hatotakiwa kufunga masiku yaliyopita kwa kuwa alikuwa ni kafiri katika masiku hayo. Kafiri haombwi kulipa matendo mema yaliyompita. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ

“Waambie waliokufuru kwamba wakikoma watasamehewa yaliyopita, lakini wakirudia, basi imekwishapita desturi ya watu wa mwanzo.” (07:38)

Jengine ni kwamba watu walikuwa wakisilimu katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala alikuwa hawaamrishi kulipa yaliyowapita katika swawm, swalah wala zakaah.

Endapo atasilimu katikati ya mchana alazimishwe kujizuia na kulipa au ajizuie pasi na kuilipa siku hiyo au sio lazima kujizuia wala kuilipa siku hiyo? Wanachuoni wametofautiana katika masuala haya. Maoni yenye nguvu ni kwamba ni lazima kwake kujizuia pasi na kulipa. Kwa hivyo ni lazima kwake kujizuia kwa kuwa amekuwa miongoni mwa watu wa wajibu. Lakini sio wajibu kwake kuilipa siku hiyo kwa kuwa kabla ya hapo hakuwa miongoni mwa watu wa wajibu. Ni kama mfano wa mtoto akibaleghe katikati ya mchana. Katika hali hii itakuwa ni wajibu kwake kujizuia na wala itakuwa sio wajibu kwake kuilipa siku hiyo kwa mujibu wa maoni yaliyo na nguvu juu ya masuala haya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/96-97)
  • Imechapishwa: 02/06/2017