Je, inajuzu kwa wanawake kuyatembelea makaburi ya al-Baqiy´ na mashahidi wa Uhud?

Swali: Je, inajuzu kwa wanawake kuyatembelea makaburi ya al-Baqiy´?

Jibu: Haijuzu kwa wanawake kuyatembelea makaburi. Bali kuyatambelea kwake makaburi ni dhambi kubwa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi sana. Hadiyth hii imepokelewa kwa njia mbili:

1- Wanawake wenye kuyatembelea makaburi sana.

2- Wanawake wenye kuyatembelea makaburi.

الزوارات ni wale wanawake wenye kuyatembelea kwa wingi. Kuhusu الزائرات  ni wale wenye kuyatembelea japokuwa mara moja. Hadiyth zote mbili ziko sawa inapokuja katika usahihi au kwa angalau zinakaribiana. Ziko katika ngazi ya uzuri. Yule mwenye kutumia dalili Hadiyth ya kwanza الزوارات analazimika kutumia dalili vilevile Hadiyth ya pili الزائرات. Kwa sababu isnadi zake ni zenye kukaribiana na ngazi zake pia zinakaribiana. Kujengea juu ya haya haijuzu kwa mwanamke kutembelea makaburi ya al-Baqiy´ na mashahidi wa Uhud.

Inafaa kwake kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makaburi ya marafiki zake wawili Abu Bakr na ´Umar? Kuna wanachuoni wenye kuonelea kuwa hapana ubaya kwake kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makaburi ya marafiki zake wawili. Kwa sababu haya sio matembezi ya kihakika. Kwa sababu hawezi kulisogelea kaburi na akasimama kaburi nalo. Kati yake yeye na kaburi kuna ukuta na hawezi kulifikia kaburi. Wapo wanachuoni wengine hawaonelei hivo midhali kuliendea kwake kunaitwa “matembezi” na yeye pia anaitakidi kuwa ni matembezi. Hili ndio salama zaidi. Asitembelee kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala makaburi ya marafiki zake wawili. Endapo atasema kuwa anataka kumtolea salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi tunamwambia amtolee salamu hapohapo alipo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Salamu zenu zinanifikia popote mnapokuwa.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (36) http://binothaimeen.net/content/797
  • Imechapishwa: 22/01/2018