Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

16- Qur-aan ni maneno ya Allaah, Uteremsho Wake na Nuru Yake. Haikuumbwa, kwa sababu Qur-aan inatokamana na Allaah na chenye kutokamana na Allaah hakikuumbwa. Hivyo ndivyo alivyosema Maalik bin Anas, Ahmad bin Hanbal na Fuqahaa´ kabla yao na baada yao.  Na kujadiliana juu yake ni kufuru.

MAELEZO

Katika I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo amezungumza kwayo kihakika. Jibriyl ameyasikia kutoka Kwake halafu akaja nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ni ´Aqiydad ambayo hakuna yeyote katika wanachuoni alienda kinyume nayo ambao wanapita juu ya Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walioenda kinyume nayo ni wapotevu katika Jahmiyyah – wafuasi wa al-Jahm bin Swafwaan – na vijukuu vya Jahmiyyah katika Mu´tazilah, Zaydiyyah, Shiy´ah na wengineo. Wote hawa wamechukua masuala haya kutoka kwa Jahmiyyah. Kadhalika Ibaadhiyyah. Wote hawa wanapita juu ya njia hii inayokwenda kinyume na mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wote wanaonelea kuwa Qur-aan imeumbwa kwa kuwa wanavyoonelea wao ni kwamba Allaah hasifiwi kuwa anazungumza kama ambavyo vilevile hasifiki kuwa na usikizi, uoni,  ujuzi, matamshi na nyenginezo. Hawamsifu kuwa ana uso, mikono miwili na nyenginezo. Malengo yao ya kufanya hivyo ni kuiharibu ´Aqiydah hata kama watajionyesha kuwa malengo yao ni kumtakasa Allaah (Jalla wa ´Alaa) kutokana na kushabihiana na viumbe. Madai haya ni ya batili. Sifa za Mola (Subhaanah) hazishabihiani na sifa za viumbe. Mola (Jalla wa ´Alaa) ana majina na sifa zinazolingana na Yeye na ukubwa na utukufu Wake. Kadhalika viumbe wana majina na sifa zinazolingana na wao na uanaadamu wao. Kwa hivyo ushabihiano kati ya aina hizo mbili si kwa njia ya uhakika na namna hata kama vitashirikiana katika maana na matamshi, lakini hata hivyo havishirikiani katika uhakika na namna. Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Dalili yao juu ya hilo ni kutoka katika Qur-aan. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

“Endapo mmoja katika washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka ayasikie maneno ya Allaah.” (09:06)

Ameyanasibisha maneno Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Amesema kuhusu wanafiki:

يُرِيدُونَ أَن يُبَدِّلُوا كَلَامَ اللَّـهِ

“Wanataka kubadilisha maneno ya Allaah.” (48:15)

Dalili kutoka katika Sunnah na maafikiano ya Ummah ni nyingi juu ya masuala haya. Ni masuala bila ya shaka ya yakini. Tofauti ya wapotevu haiathiri kitu juu ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah. Qur-aan ni sehemu katika maneno ya Allaah (Subhaanah). Allaah anazungumza na bado ni Mwenye kuendelea kuzungumza akitakacho na pale anapotaka. Anasifika kuzungumza. Qur-aan hii ni sehemu katika maneno ya Allaah. Amezungumza kwa Tawraat na kadhalika akaiandika kwa mikono Yake. Vilevile [amezungumza] kwa Injiyl, az-Zabuur, anazungumza kwa maamrisho na makatazo. Hakika Yeye hukiambia kitu “Kuwa!” na kinakuwa papo hapo:Ameyanasibisha Kwake.

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika amri Yake Yeye akitaka kitu chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.” (36:82)

Amejithibitishia Mwenyewe maneno.

إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَىٰ

“Pindi aliposema Allaah: “Ee ‘Iysaa… ” (03:55)

Vilevile amemzungumzisha Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno ambayo Muusa aliyasikia wakati alipomtuma kwa Fir´awn. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasifika kwa maneno. Miongoni mwa maneno Yake ni Qur-aan Tukufu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 22/01/2018