Swali: Tunafanya katika katika dula la kuuza nguo. Katika mwezi wa Ramadhaan kumi la mwisho hatuwezi kukaa I´tikaaf wakati wa mchana kutokana na mazingira ya kazi. Je, ni sahihi kukaa I´tikaaf wakati wa usiku peke yake na mchana tukafanya kazi dukani?

Jibu: Inafaa kufanya I´tikaaf ijapo kitambo fulani cha muda ndani ya msikiti ambao kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko. Ni sahihi kufanya I´tikaaf kama mtu hakufunga kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. ´Abdullaah bin ´Umar amepokea kupitia kwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi kipindi kabla ya Uislamu niliweka nadhiri ya kukaa I´tikaaf usiku mmoja katika msikiti Mtakatifu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Tekeleza nadhiri yako!” Akafanya I´tikaaf usiku mmoja.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim katika ”as-Swahiyh” zao na tamko hili ni la al-Bukhaariy (02/260). Kama swawm ingelikuwa ni sharti ya kusihi kwa I´tikaaf, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingemkubalia kufanya I´tikaaf wakati wa usiku peke yake. Kwa hivyo inafaa kwenu kuweka kikomo cha nia ya kukaa I´tikaaf wakati wa usiku peke yake pasi na mchana kutokana na mliyotaja. Mnapata thawabu kwa kiasi chenu – Allaah akitaka.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Lajnah ad-Daaimah (09/321) nr. (18979)
  • Imechapishwa: 23/04/2022