Israfu inayofanya ya kumwaga chakula wakati wa maharusi na kuwakirimu wageni

Swali: Kwa mnasaba wa likizo ya majira ya joto napenda kukuwekea wazi tatizo ambalo wanatumbukia ndani yake watu wengi; nalo ni kuhusiana na minasaba. Kuna baadhi ya watu wanaotaka kuwakirimu wageni ambapo wanachinja kichinjwa ambacho kinakuwa ni ziada ya haja na kile kilichobaki wanakitupa. Ni zipi nasaha zako kwa watu hawa khaswa hivi ambapo tunakaribia misimu ya ndoa na mfano wa hayo? Je, una nasaha zozote za kuwapa watu hawa? Je, una nasaha kwa wale ambao hawafurahi isipokuwa mpaka wachinje na hawatosheki na chakula kingine?

Jibu: Nasaha kwa yule ambaye anataka kumkirimu mgeni tunamwambia kwamba endapo wageni watakuwa ni wengi hakuna neno. Hili ni bora kuliko kwenda na kununua nyama. Ama mgeni akiwa mmoja au wawili basi usichinje. Kwa sababu huku ni kufanya israfu ambako Allaah amekataza pale aliposema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ

“Kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Kwani Yeye hapendi wanaofanya israfu.”[1]

Iwapo tutakadiria kuwa yule mgeni aliyepata mtu ni mgeni mkubwa aliye na hadhi ni sawa kumchinjia kichinjwa ikiwa utawapata watu ambao wanaweza kufaidika nacho baada ya kumkirimu mgeni. Kama ambavyo Answaar walivyomchinjia kichinjwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipokuja kama mgeni akiwa pamoja na Abu Bakr na ´Umar. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Tahadhari na maziwa.”

Akamuidhini kuchinja. Lakini ni jambo linalotambulika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyama wala chakula vilikuwa havitupwi. Watu walikuwa wakinufaika nacho.

Kuhusiana na yule mgeni ambaye haoni kuwa amekirimiwa mpaka tu achinjiwe, namnasihi aachane na ujinga huu. Haya ni katika matendo ya kile kipindi kabla ya kuja Uislamu. Kumkirimu mgeni kunakuwa kwa mujibu wa desturi za watu midhali hakuna israfu ndani yake. Usiwatie watu uzito wakukirimu kwa kukuchinjia. Inatosha wakikupokea kwa uso mkunjufu, moyo mkunjufu, wakaongea nawe vizuri na salamu. Haya yanatosha.

[1] 07:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (36) http://binothaimeen.net/content/793
  • Imechapishwa: 22/01/2018