Inajuzu kula chakula cha mayahudi na manaswara, kuswali majumbani mwao na kuingia kanisani?

Swali: Baadhi ya marafiki wa kinaswara masomoni wananiita manyumbani mwao ili kuchangia nao chakula. Je, inajuzu kwangu kula katika chakula chao ikithibiti kwangu kuwa ni halali katika Shari´ah?

Jibu: Ndio, inajuzu kula kwenye chakula kinachokupa rafiki yako mnaswara, sawa kikiwa katika nyumba yake au nyumba nyingine, ikikuthibitikia kuwa chakula hiki kwa dhati yake sio haramu au hali yake haijulikani. Kwa sababu asli ni kujuzu mpaka ithibiti dalili yenye kukataza. Kuwa kwake mnaswara sio kizuizi. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) ametuhalalishia chakula cha Ahl-ul-Kitaab.

Swali B: Je, inajuzu kwangu kuwapa vitabu vilivyo na Aayah tukufu vyenye kuthibitisha upwekekaji wa Allaah (Ta´ala) vilivyoandikwa kwa kiarabu na kutarjumiwa maana yake kwa kingereza?

Jibu: Ndio, inajuzu kuwapa vitabu vilivyo na Aayah za Qur-aan zenye kutolea dalili juu ya hukumu, Tawhiyd na mengineyo. Ni mamoja vikawa katika lugha ya kiarabu au vimetarjumiwa maana yake. Bali unashukuriwa kwa hilo kwa kuwa kuwapa navyo ili wasome ni aina moja ya kufikisha na kulingania katika dini ya Allaah. Mwenye kufanya hivo analipwa ujira akiitakasa nia yake.

Swali C: Wakati fulani swalah inafika na mimi niko kwenye nyumba ya mmoja wao. Hivyo nachukua mkeka wao maalum na naswali mbele yao. Je, swalah yangu ni sahihi kwa vile niko katika nyumba yao?

Jibu: Ndio, swalah yako inasihi. Allaah akuzidishie hima ya kumtii na khaswa kutekeleza swalah tano kwa wakati wake. Lililo la wajibu ni kufanya bidii kuziswali katika mkusanyiko na kuimarisha kwazo misikiti kiasi na utakavyoweza.

Swali D: Wameniomba kwenda nao kanisani na nikakataa mpaka kwanza niulize juu ya hukumu ya hili. Je, inajuzu kwenda nao ili niweze kuthibitisha upwekekaji ulioko katika Uislamu na kwamba ni dini ya walimwengu na ili waweze kuitikia Uislamu? Haya na khaswa ukizingatia kuwa dini yao ni ya kinaswara na madhehebu yao ni protestanti. Wanasema kuwa katika maombi yao hawana Sujuud wala Rukuu´. Pamoja na kuwa mimi kwangu ni jambo katu katu lisilowezekana nikaingia katika dini ya kinaswara kwa idhini ya Allaah (Ta´ala).

Jibu: Ikiwa kwenda kwako nao kanisani ni kwa lengo la kudhihirisha kusameheana na usahali haijuzu. Ama lengo ikiwa ni kuwalingania katika Uislamu na ukawa haushirikiani nao katika ´ibaadah zao na huchelei kuathirika na ´ibaadah zao, ada zao na mambo yao inajuzu.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (75-76/02)