Imamu kukusanya Rakaa´ nne pamoja kwa Tasliym moja katika Tarawiyh

Swali: Baadhi ya maimamu wanakusanya Rakaa´ nne au zaidi katika swalah ya Tarawiyh kwa Tasliym moja pasi na kuketi baada ya Rakaa´ mbili na huku wanadai kuwa ni Sunnah. Je, kitendo hichi kina msingi katika Shari´ah yetu safi?

Jibu: Kitendo hichi hakikuwekwa katika Shari´ah. Bali kimechukizwa au ni haramu kwa mtazamo wa wanachuoni wengi kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah ya usiku ni mbili mbili.”[1]

Kumeafikiana juu yake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Imethibiti vilevile kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Rakaa´ kumi na moja ambapo akileta Tasliym kila baada ya Rakaa´ mbili na akiwitiri kwa Rakaa´ moja.”[2]

Kumeafikiana juu ya usahihi wake.

Hadiyth zilizo na maana kama hii ni nyingi.

Kuhusu Hadiyth ya ´Aaishah inayotambulika:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali usiku [Rakaa´] nne; usiulize juu ya uzuri wake na urefu wake, kisha anaswali [Rakaa´] nne; usiulize juu ya uzuri wake na urefu wake.”

Kumeafikiana juu yake.

makusudio ni kwamba alikuwa akitoa salamu kila baada ya Rakaa´ mbili. Makusudio si kwamba alikuwa akizifululiza zote mbili kwa salamu moja kutokana na Hadiyth iliotangulia. Hayo ni kutokana na yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah ya usiku ni mbili mbili.”[3]

kama tulivyotangulia kusema. Hadiyth baadhi inazisadiki zengine na baadhi inazifasiri zengine. Ni wajibu kwa muislamu kuzitendea kazi zote na kufasiri zile zilizokuja kwa njia ya ujumla kutokana na zile zilizo wazi.

[1] al-Bukhaariy (472) na Muslim (749).

[2] Muslim (736).

[3] al-Bukhaariy (472) na Muslim (749).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/38-39)
  • Imechapishwa: 23/05/2018