Imamu amewaswalisha watu bila wudhuu´


Swali: Imamu amewaswalisha watu na katikati ya swalah akakumbuka kuwa hana wudhuu´. Akakamilisha kuwaswalisha kisha akarudi kuiswali peke yake na wala hakuwafahamisha waswaliji jambo hilo.

Jibu: Haijuzu kwake kufanya hivo. Ni lazima kwake atapokumbuka kuwa hana wudhuu´ basi arudi nyuma na amtangulize ambaye atawakamilishia swalah yao. Anaweza vilevile kukata swalah na akarudi kuiswali upya. Kwa sababu wanachuoni wametofautiana juu ya masuala haya. Hanaabilah wanaona kuwa akitanguliwa na hadathi basi haifai nafasi yake akaweka niaba mwingine. Anachotakiwa kufanya ni yeye kukata swalah na wamsubiri mpaka atakapotawadha na waanze swalah upya au amtangulize mwingine. Lakini akiwa na wudhuu´ lakini akahisi kuwa hawezi kuendelea na hali hiyo imemtokea kabla ya wudhuu´ wake kuchenguka, basi arudi nyuma kisha amtangulize mbele ambaye anaweza kuwakamilishia swalah yao. Wanachuoni wengine wakaona kuwa inafaa kwake nafasi yake kuweka niaba mwingine. Ni mamoja ametanguliwa na hadathi au hakutanguliwa na hadathi. Haya ndio madhehebu ya maimamu watatu. Dalili ya hayo ni Hadiyth ya al-Bukhaariy:

“Wawaongozeni katika swalah; – bi maana maimamu wenu – wakipatia, basi mmepatia nyinyi na wao wamepatia na wakikosea, basi nyinyi mmepatia na itakuwa dhidi yao.”

Kwa kufupiza ni kwamba wale waumini ambao hawatojua [kwamba imamu amechengukwa na wudhuu´] basi swalah yake ni sahihi. Lakini kilicho wajibu kwa imamu ni yeye kukata swalah na haijuzu kwake kuendelea.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (15)
  • Imechapishwa: 10/09/2020