Ni Ibn ´Abdir-Rahmaan. Imaam, Haafidhw, Shaykh-ul-Islaam na mwanachuoni wa Misri. Ni Abul-Haarith al-Fahmiy, mtumwa aliyeachwa huru na Khaalid bin Thaabit bin Dhwaa´in.

Familia yake wanasema kuwa ni wafursi wanaotokamana na Aswbahaan na wala hakuna mgongano wowote kati ya kauli hizo mbili.

Alizawa Qarqashandah kusini mwa Misri.

al-Layth (Rahimahu Allaah) alikuwa Faqiyh wa Misri, Muhaddith na kiongozi mzuri, ambaye mtu anajifakhari kwa kutoka mji mmoja kama yeye. Viongozi wa Misri, mahakimu, mawaziri na wale waliokuwa chini ya amri yao daima walikuwa wakirejea katika maoni na ushauri wake. al-Mansuur alikuwa anataka kumfanya kuwa naibu wake, lakini akaomba udhuru na akakataa.

Sa´iyd bin Abiy Maryam amesema: “Nimemsikia al-Layth bin Sa´d akisema:

“Nimefikisha miaka thamanini na kamwe sijawahi kujadili na mtu anayefuata matamanio.”

Nasema: Ahl-ul-Ahwaa´ wal-Bid´ah walikuwa wanyonge katika zama za al-Layth, Maalik na al-Awzaa´iy na Sunnah ilikuwa na nguvu na yenye kutukuzwa. Lakini katika zama za Ahmad bin Hanbal, Ishaaq na Abu ´Ubayd Bid´ah zikaanza kudhihiri na wakatahiniwa maimamu wa Sunnah. Ndipo Ahl-ul-Ahwaa´ wakanyanyua vichwa vyao kwa sababu ya kuwa na nchi. Wanachuoni wakahitaji kuhojiana nao kwa Qur-aan na Sunnah. Kisha wakaongezeka. Kadhalika wanachuoni wakahojiana nao kwa kutumia akili. Mahojiano yakawa marefu na tofauti zikapamba moto na hoja tata zikazalika – tunamuomba Allaah msamaha.

Ibn Bukayr amesema: “Nimemsikia al-Layth akisema:

“Mwaka 113 nilikuwa Makkah na nikasikia [Hadiyth] kutoka kwa az-Zuhriy. Kipindi hicho nilikuwa na miaka 20.”

´Iysaa bin Zughbah amesema: “Nimemsikia al-Layth akisema:

“Asili yetu ni kutokea Aswbahaan.”

Yahyaa bin Bukayr amesema: “Nimepewa khabari na mtu aliyemsikia al-Layth akisema:

“Niliingia kwa Naafiy´ akaniuliza ni wapi ninapotokea. Nikasema: “Misri.” Akasema: “Kutokamana na nani?” Nikasema: “Kutokamana na Qays.” Akasema: “Una miaka mingapi?” Nikajibu: “Miaka 20.” Ndipo akasema: “Lakini una ndevu kama za ambaye ana miaka 40.”

al-Layth amesema:

“Abu Ja´far alinambia: “Unataka kutawala Misri?” Nikasema: “Hapana, ee kiongozi wa waumini. Mimi ni mnyonge zaidi wa hilo. Mimi ni mtumwa niliyeachwa huru.”Ndipo akasema: “Wewe si mnyonge pamoja nami, lakini nia yako ndio imedhoofika kunifanyia kazi.”

Yahyaa bin Bukayr amesema: “Nilikutana na watu masiku ya mtawala Hishaam. Kipindi hicho al-Layth bin Sa´d alikuwa bado kijana mdogo. Wakati huo alikuweko Misri ´Ubaydullaah bin Abiy Ja´far, Ja´far bin Rabiy´ah, al-Haarith bin Yaziyd, Yaziyd bin Abiy Habiyb na Ibn Hubayrah. Wote walikuwa wakitambua fadhilah za al-Layth, uchaji wake na uzuri wa Uislamu wake licha ya miaka yake midogo.” Kisha Ibn Bukayr akasema:

“Sijapata kuona mtu mfano wa al-Layth.”

Yahyaa bin Bukayr amesema:

“Sijawahi kumuona mtu ambaye ni mkamilifu zaidi kama al-Layth.”

Ibn Wahb amesema:

“Lau kama si Maalik na al-Layth, basi watu wangelipotea.”

Ibn Wahb amesema:

”Lau kama si Maalik na al-Layth, basi ningelipotea. Nilikuwa nafikiri kuwa mtu anatakiwa kutendea kazi kila kilichonasibishwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

´Uthmaan bin Swaalih amesema:

”Wamisri walikuwa wakimponda ´Uthmaan mpaka pale al-Layth alipozuka kati yao. Ndipo akaanza kuzungumzia fadhilah zake jambo lililowafanya kukomeka. Watu wa Himsw walikuwa wakimponda ´Aliy mpaka pale Ismaa´iyl bin ´Ayyaash alipozuka kati yao. Ndipo akaanza kuzungumzia fadhilah za ´Aliy jambo lililowafanya kukomeka.”

Harmalah amesema:

”Kila mwaka al-Layth alikuwa akimtumia Maalik dinari 100. Siku moja Maalik akamwandikia: ”Nina deni.” Ndipo al-Layth akamwagizia dinari 500.”

Mwanamke mmoja alikuja kwa al-Layth akasema:

”Ee Abul-Haarith! Nina mvulana mgonjwa anayehitaji asali.”Akasema [kumwambia mvulana yule]: “Ee kijana! Mpe Mirtw asali.”

Mirtw ni lita 120.

´Abdullaah bin Swaalih amesema:

”Tulitoka safari pamoja na al-Layth kwenda Alexandria [al-Iskandariyyah] na alikuwa na safina tatu. Safina moja ilikuwa na nyama zake, safina nyingine ilikuwa na familia yake na safina nyingine ilikuwa na wageni wake. Ulipokuwa unafika wakati wa swalah basi alikuwa anaenda nchi kavu na akiswali.”

al-Layth amesema:

”Nilikuwa al-Madiynah pamoja na mahujaji na huko kulikuwa na taka nyingi. Nilikuwa nikivaa khofu zangu. Ninapofika mlango wa msikiti basi huzivua na kuingia ndani. Ndipo Yahyaa bin Sa´iyd al-Qattwaan akasema: “Usifanye hivo. Kwani hakika wewe ni imamu ambaye watu wanakutazama.” Anakusudia kuvaa khofu.”

al-Fadhwl bin Ziyaad amesema:

“al-Layth ni mwenye elimu nyingi na Hadiyth zilizo Swahiyh.”

al-A´alaa´ bin Kathiyr amesema:

”al-Layt bin Sa´d ndiye bwana, imamu na mwanachuoni wetu.”

Yahyaa bin Bukayr na Sa´iyd bin Abiy Maryam amesema:

”al-Layth alifariki tarehe kumi na tano mwaka 175.”

Yahyaa amesema:

”Ilikuwa siku ya ijumaa. Muusa bin ´Iysaa alimswalia swalah ya jeneza.”

Sa´iyd amesema:

“Alikufa usiku wa kuamkia ijumaa.”

Khaalid bin ´Abdis-Salaam as-Sadfiy amesema:

“Nilishuhudia mazishi ya al-Layth bin Sa´d pamoja na baba yangu. Sijawahi hapo kabla yake kuona mazishi yaliyokuwa na watu wengi. Watu wote walikuwa na huzuni na wakipeana pole kwa kulia. Nikasema: ”Ee baba, ni kana kwamba kila mtu ana udugu na aliyekufa huyu.” Akasema: ”Ee mwanangu, kamwe hutoona tena mfano wake.”

al-Waliyd bin Muslim amesema:

“Nilimuuliza Maalik, ath-Thawriy, al-Layth na al-Awzaa´iy juu ya maelezo yanayozungumzia Sifa ambapo wakasema:

“Zipitisheni kama zilivyokuja.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (8/136-164)
  • Imechapishwa: 15/10/2020