Ni Ibn Mas´uud bin Bishr. Imaam, kiigizo, imara na Shaykh-ul-Islaam. Abu ´Aliy at-Tamiymiy al-Yarbuu´iy al-Khuraasaaniy. Alikuwa jirani na msikiti Mtakatifu. Alizaliwa Sarmakand, akakulia Abiyward na akasafiri kwa ajili ya kutafuta elimu.

Kuufah aliandika kwa Mansuur, al-A´mash, Yahyaa bin Sa´iyd al-Qattwaan, Ibn Abiy Laylaa, Ja´far as-Saadiq na wengineo.

Baadhi ya waliohadithia kutoka kwake ni pamoja na Ibn-ul-Mubaarak, Yahyaa al-Qattwaan, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, Ibn ´Uyaynah, ´Abdur-Razzaaq, ash-Shaafi´iy, Yahyaa bin Yahyaa at-Tamiymiy na Ibn Wahb.

al-Fadhwl bin Muusa amesema:

”al-Fudwayal bin ´´Iyaadhw alikuwa mtu mwenye busara akiwapora watu kati ya njia ya Abiyward na Sarkhas. Sababu ya kutubu kwake ni kwamba alimpenda mjakazi mmoja. Siku moja wakati alipokuwa akipanda juu ya ukuta akamsikia mtu mmoja akisoma:

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ

“Je, hivi haujafika wakati kwa wale walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao juu ya kumtaja Allaah?”[1]

Aliposikia hivo akasema:

”Ndio, Mola, umefika wakati.”

Ndipo akatubu. Usiku ulipofika akaenda kujihifadhi kwenye gofu. Tahamaki akawakuta wasafiri wako ndani yake. Baadhi yao wakasema waendelee na safari na wengine wakasema:

”Hapana, tusubiri mpaka kuingie asubuhi. Hivi sasa al-Fudhwayl yuko barabarani akiwapora watu.”

Ndipo akasema:

”Nikafiri na kujiambiwa nafsi yangu: ”Mimi usiku mzima nakesha kwenye maasi na hapa kikosi cha waislamu kina khofu juu yangu. Hakuna sababu nyingine Allaah amenifanya kuja kukaa hapa isipokuwa ni kwa sababu anataka mimi kuachana na jambo hilo. Ee Allaah! Hakika nimetubu Kwako na nimeifanya tawbah yangu kuwa jirani na Msikiti Mtakatifu.”

Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

”al-Fudhwayl ni mwaminifu.”

Ibn Mahdiy amesema:

” al-Fudhwayl ni mtu mwema, lakini hakuwa hafidhi.”

al-´Ijliy amesema:

”Alikuwa anatokea Kuufah. Mwaminifu mfanya ´ibaadah. Alikuwa ni mtu mwema akiishi Makkah.”

an-Nasaa´iy amesema:

”Alikuwa mwaminifu, mwenye kuaminiwa  na mtu mwema.”

ad-Daaraqutwniy amesema:

“Mwaminifu.”

Ibn-ul-Mubaarak amesema:

“Sijaona mtu juu ya uso wa ardhi ambaye ni bora kumshinda al-Fudwayl bin ´Iyaadhw.”

Abu Muhammad bin Muzaahim amesema:

“Nimemuona mtu mwenye kufanya ´ibaadah kwa wingi; ´Abdul-´Aziyz bin Rawwaad, mtu mwenye uchaji zaidi; al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw, mtu mjuzi zaidi; Sufyaan ath-Thawriy na bingwa zaidi wa Fiqh; Abu Haniyfah. Sijamuona mtu katika Fiqh mfano wake.”

Ibraahiym bin al-Ash´ath amesema:

“Sijamuona mtu ambaye Allaah ndani ya moyo wake alikuwa mtukufu zaidi kama al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw. Alikuwa anampotaja Allaah, akatajwa mbele yake au akasikia Qur-aan, basi anaonekana kuingiwa na khofu na huzuni na macho yake yakajawa na machozi na akalia mpaka akaonewa huruma na yule aliye pembezoni mwake. Daima alikuwa mwenye huzuni na mwenye kufikiria kwa wingi. Ilikuwa tunapotoka kwenda kazika mazishi basi anaendelea kutoa mawaidha, akifanya Adhkaar na akilia kama kwamba anawaaga marafiki zake kwa ajili ya kwenda Aakhirah, mpaka afike makaburini. Akikaa kati ya wafu na akihuzunika na akilia mpaka wakati wa kuinuka kana kwamba amerejea kutoka Aakhirah.”

al-Fudhwayl amesema:

“Yule mwenye kumwogopa Allaah hatodhuriwa na yeyote na yule mwenye kumwogopa mwingine asiyekuwa Allaah hatonufaishwa na mwengine.”

al-Fudhwayl amesema:

“Khofu ya mja kwa Allaah ni kwa kiwango cha utambuzi wake juu ya Allaah. Na kuipa kwake nyongo dunia ni kwa kiasi cha vile anavyoitamani Aakhirah. Yule mwenye kutendea kazi kwa yale anayoyajua basi hahitajii yale asiyoyajua na yule mwenye kutendea kazi kwa yale anayoyajua, basi Allaah atamwongoza kwa yale asiyoyajua. Yule ambaye tabia yake itakuwa mbaya basi dini yake itakuwa mbaya, ufikiriaji wake na heshima yake.”

al-Fudhwayl amesema:

“Mambo yalivyo ni kwamba jana ni mfano tu, leo ni kitendo na kesho ni matumaini.”

 al-Fudhwayl amesema:

“Naapa kwa Allaah si halali kwako kumuudhi mbwa wala nguruwe pasi na haki. Ni vipi basi umuudhi muislamu?”

al-Fudhwayl amesema:

“Mja hatokuwa ni katika wenye kumcha Allaah mpaka ampe amani adui yake.”

al-Fudhwayl amesema:

“Lau ningepewa chaguo kati ya kuishi kama mbwa na kufa kama mbwa pasi na kukutana na siku ya Qiyaamah, basi ningechagua hili la pili.”

 al-Fudhwayl amesema:

“Allaah akimpenda mja, basi hufanya misononeko yake kuwa mingi zaidi, na anapomchukia mja, basi humkunjulia zaidi dunia yake.”

al-Fudhwayl amesema:

“Yule anayependa kukumbukwa basi hatokumbukwa na yule anayechukia kukumbukwa basi atakuja kukumbukwa.”

 al-Fudhwayl amesema:

“Ni nini kuipa nyongo dunia?” Akajibu: “Kukinaika.” Kukasemwa: “Ni nini kujichunga?”Akajibu: ”Kuyaepuka mambo ya haramu.” Kukasemwa: ”Ni nini ´ibaadah?” Akajibu: ”Kutekeleza yale mambo ya faradhi.” Kukasemwa: ”Ni nini kunyenyekea?” Akajibu: ”Kunyenyekea haki.” Kujichunga zaidi kuliko mdomoni.”

al-Fudhwayl amesema:

“Usipoweza kusimama usiku na kushinda mchana umefunga, basi tambua kuwa wewe ni mwenye kukoseshwa. Janga lako ni yale madhambi yako.”

al-Fudhwayl amesema:

“Mjinga anasamehewa dhambi sabini ambazo mfano wake mwanazuoni hasamehewi dhambi hata moja.”

al-Fudhwayl amesema:

“Yule mwenye kumpenda mzushi basi Allaah atayaporomosha matendo yake na ataondosha nuru ya Uislamu moyoni mwake.”

 Ibraahiym bin al-Ash´ath amesema: “Nimemsikia al-Fudhwayl akisema alipokuwa katika hali ya kukata roho:

“Nionee huruma. Hakuna kitu ninachopenda kukushinda Wewe.”

al-Fudhwayl amesema:

“Mambo mawili yanaufanya moyo kuwa msusuwavu; kuongea sana na kula sana.”

Ni katika watu wa kizazi cha Sufyaan bin ´Uyaynah lakini alifariki miaka kadhaa kabla yake.”

[1] 57:16

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (8/421-448)
  • Imechapishwa: 24/09/2020