Zuhayr bin Harb bin Shaddaad al-Harashiy an-Nasaa´iy kisha al-Baghdaadiy. Hafidhi na hoja na mmoja katika wanachuoni wanaojulikana katika Hadiyth. Ni huri wa Banuu al-Haarish bin Ka´b bin ´Aamir bin Sa´sa´h. Baba yake alikuwa anaitwa Ashtaal na akalifanya kiarabu “Shaddaad”.

Baada ya kusafiri sana kutafuta elimu, akafanya makazi Baghdaad ambapo akakusanya, akatunga na akatukuza elimu hii yeye pamoja na mwanae na mjukuu wake Muhammad bin Ahmad.

Abu Khaythamah alizaliwa mwaka 160 kwa mujibu wa mwanae Abu Bakr.

Baadhi ya waliohadithia kutoka kwake ni Sufyaan bin ´Uyaynah, Wakiy´, Yahyaa al-Qattwaan, Yaziyd bin Haaruun, Hafsw bin Ghayyaath, ´Abdur-Razzaaq, Ibn ´Ulayyah na wengineo.

Miongoni mwa wale waliopokea kutoka kwake ni pamoja na al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, Ibn Maajah, an-Nasaa´iy, Abu Zur´ah, Abu Haatim, Ibn Abiyd-Dunyaa, Baqiyy bin Makhlad, Abu Ya´laa al-Muusuliy, Muusa bin Haaruun na wengineo.

Amefanywa kuwa mwaminifu na Yahyaa bin Ma´iyn.

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

“Abu Khaythamah anatosha kwa kabila nzima.”

Abu Haatim amesema:

“Mwaminiwa.”

Abu ´Ubayd amesema:

“Nilisema kumwambia Abu Daawuud: “Abu Khaythamah ni hoja juu ya wanamme?” Akasema: “Ni uzuri ulioje wa elimu yake.”

an-Nasaa´iy amesema:

“Mwaminifu na mwaminiwa.”

al-Husayn bin Quhm amesema:

“Mwaminifu na imara.”

al-Khatwiyb al-Baghdaadiy amesema:

“ Alikuwa mwaminifu, imara, hafidhi na mairi.”

Abu Bakr amesema:

“Baba yangu alifariki katika ukhaliyfah wa al-Mutawakkil usiku wa kuamkia alkhamisi tarehe ishini na tatu Sha´baan mwaka 234. Alikuwa na miaka 74 – Allaah amrehemu.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/489-492)
  • Imechapishwa: 22/09/2020