Swali: Mimi natokea Dammaam sehemu za mashariki. Kazini kwangu wapo karibu 90% Raafidhwah. Wanakula, wanakunywa, wanafanya kazi na wanaishi pamoja nasi. Kadhalika wanaswali pamoja nasi katika misikiti. Ni ipi hukumu ya kuchanganyikana nao, kula na kufanya nao kazini?

Jibu: Raafidhwah hawa wanasema kuwa ni waislamu. Sivyo?

Muulizaji: Ndio, wanasema kuwa ni waislamu…

Ibn ´Uthaymiyn: Na wewe pia ni muislamu. Sivyo? Walinganie katika ule Uislamu wa haki. Ni lazima kwako kuwalinganie katika ule Uislamu ambao unaona kuwa ni haki. Lakini unatakiwa kufanya hivo pasi na kuwafanyia ukali juu ile batili waliyomo. Walinganie katika Uislamu. Waeleze juu ya Qur-aan na kwamba hakukupungua herufi hata moja ndani yake na wala hakukuzidishwa ndani yake herufi hata moja. Waeleze juu ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah waongofu na kadhalika.

Mtu akilingania kwa Allaah kwa imani safi na akabainisha haki, basi yataonekana matunda. Ulinganizi wake utakuwa na faida. Ama kumwendea mtu na akamshambulia juu ya Bid´ah zake hata kama itakuwa ukafiri na akasema kuwa anafanya hivo kwa sababu ya ghera na kwamba ni mwenye kulingania kwa Allaah, basi hatonufaisha kitu. Hakuna kitachozidi isipokuwa uadui na chuki. Hakuna ambaye ni mwenye hekima zaidi kuliko Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ

“Je, kwani Allaah si mwadilifu zaidi wa wanaohukumu kuliko mahakimu wote?”[1]

Ametwambia:

وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ فَيَسُبُّوا اللَّـهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ

“Na wala msiwatukane wale wanaowaomba badala ya Allaah wasije nao kumtukana Allaah kwa uadui bila ya elimu.”[2]

Ni lazima kwenu kuwalingania katika ule Uislamu wa haki pasi na kushambulia juu ya yale waliyomo katika zile ´Aqiydah mbovu ili waweze kuhisi raha na wakubali:

“Allaah kumwongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”

Muulizaji: Wanaswali pamoja nasi misikitini.

Ibn ´Uthaymiyn: Ni vizuri. Wakiswali pamoja nasi misikitini, basi imamu wa msikiti achague kitabu kinachozungumzia maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Muulizaji: Wanaswali juu ya makaratasi na udongo uliotengenezwa…

Ibn ´Uthaymiyn: Haya ni mambo ya mataga. Yakiwa hayakufungamana na ´Aqiydah za kishirikina, basi haya ni mambo tu ya kimataga. Kwa mfano hivi sasa wako watu ambao hawanyanyui mikono yao wanapoenda katika Rukuu´, wanaponyanyuka kutoka hapo na wanaponyanyuka kutoka katika Rak´ah ya pili kwenda ya tatu. Sambamba na hilo wako watu ambao wananyanyua mikono yao katika kila hatua. Kila mmoja anadai kuwa anafata haki. Mambo ya mataga jambo lake ni sahali. Lengo ni kuzioanisha nyoyo juu ya haki na kwamba mtu afate njia nyepesi zaidi inayofikisha huko. Je, pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anawalingania watu katika haki alikuwa akianza kushambulia ile batili waliyomo? Alikuwa akianza kuwalingania katika Uislamu. Mimi sikatai mtu kuwa na ghera juu ya Uislamu. Napendelea mtu awe na ghera itakayomfanya kuchukia kila kitu kisichokuwa haki. Hata hivyo napenda awe na hekima wakati anapolingania katika haki.

[1] 95:08

[2] 06:108

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (187 B) Tarehe: 1419-06-04/1998-09-25
  • Imechapishwa: 27/09/2021