Ibn ´Uthaymiyn utoko unaotoka kwenye tupu ya mwanamke


Swali: Ni upi usahihi wa kanuni hii:

”Kila chenye kutoka kupitia tupu ya mbele na ya nyuma kinachengua wudhuu´.”?

Inajuzu kwa mwanamke ambaye anatokwa na utoko kufanya kama anavyofanya mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa ambapo akakusanya kati ya swalah mbili?

Jibu: Kanuni hii inayosema:

”Kila chenye kutoka kupitia tupu ya mbele na ya nyuma kinachengua wudhuu´.”

imechukuliwa kutoka katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… asitoke mpaka asikie sauti au ahisi harufu yake.”

Bi maana yule mwenye kutilia shaka kama ametokwa na pumzi au hapana. Katika hali hii asitoke mpaka pale ataposikia sauti au akahisi harufu yake.

Ni jambo linalojulikana ya kwamba upepo huu hauna neno na kwamba una harufu tu. Ikiwa upepo huu ambao hauna neno na si vyengine isipokuwa tu una harufu unachengua wudhuu´, basi kitu kilicho na neno ni kibaya zaidi kuliko upepo huo na kinachengua wudhuu´.

Lakini naona kuwa utoko huu ambao unamtoka mwanamke siku zote, japokuwa unachengua wudhuu´, lakini hata hivyo ni kitu kisafi. Halazimiki kuosha nguo zake kutokamana nao.

Kuhusu kujuzu kwake kukusanya kati ya swalah mbili kutokana na usumbufu anaopata wa kutawadha kunapoingia kila swalah ni jambo linalofaa. Kwa msemo mwingine ni kwamba inafaa kwake kukusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa ikiwa anahisi uzito wa kutawadha kunapoingia kila swalah. Ama ikiwa hahisi uzito wowote basi lililo la wajibu ni yeye kuswali kila swalah kwa wakati wake. Ikibidi kukusanya swalah atakusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Hata hivyo asizifupishe. Kufupisha ni pale mtu anapokuwa safarini tu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (30)
  • Imechapishwa: 23/10/2017