Ibn ´Uthaymiyn mwanamke kunyoa nywele za mapajani na mikononi

Swali: Kuna mwanamke ambaye ni mwaminifu kwetu huja nyumbani kwetu tukimwita ambapo hutunyoa nywele za kwenye mikono na kwenye mapaja. Je, inajuzu kwake kuona mapaja yangu? Kwa sababu nimekusikia kwenye mkanda kwa anwani “Naswaa-ih ´Aammah” ukisema kwamba haijuzu kwa mwanamke kutazama ´Awrah ya mwanamke. Je, hali kama hii ni dharurah?

Jibu: Hali hii sio dharurah. Kwa sababu kuondosha nywele za kwenye mapaja na kwenye mikono uhalali wake unahitajia kuangaliwa vizuri. Kwa sababu nywele hizo ni katika uumbaji wa Allaah. Kugeuza uumbaji wa Allaah – katika mambo ambayo hakuyaidhinisha – ni katika kazi ya shaytwaan. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu shaytwaan:

وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ

“… na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah.”[1]

Nywele zinaingia katika uumbaji wa Allaah. Kwa hivyo haziondoshwi isipokuwa tu zile ambazo kumeruhusiwa kuziondosha. Mfano wa nywele hizo ni kama za sehemu za siri, makwapa, masharubu – hili linamuhusu mwanaume – hizi ndio zinaondoshwa. Kuhusu nywele za kwenye mikono na kwenye mapaja zisiondoshwe.

Lakini hata hivyo lau mwanamke atakuwa na nywele nyingi kiasi cha kwamba nywele zake za mguuni zitakuwa kama za mwanaume ni sawa akaziondosha. Ama nywele zikiwa nyingi kwenye mapaja asinyolewe nazo na mwanamke mwingine. Anatakiwa kuzinyoa mwenyewe. Hakuna haja ya kumtaka usaidizi mwanamke mwingine. Leo kuna vifaa vingi vya kunyolea nywele kiasi cha kwamba ukiweka juu ya nywele tu zinaondoka. Vitumiwe vifaa hivi kwa sharti mtu arejee kwanza kwa daktari.

Kwa kukhitimisha ni kwamba zisinyolewe nywele ambazo hakukuamrishwa kuzinyoa. Isipokuwa tu ikiwa kama zitakuwa nyingi kwa nisba ya mwanamke na zikawa kama nywele za mwanaume. Katika hali hii anaruhusiwa kuzinyoa. Hakuna haja ya kutaka msaada kutoka kwa mwanamke amsaidie kumnyoa nazo kwa sababu leo vifaa vya kunyolea vinapatikana kwa urahisi. Kwa hivyo hana haja ya kumtaka msaada mwanamke mwingine.

[1] 04:113

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (13)
  • Imechapishwa: 01/10/2017