Ibn ´Uthaymiyn msafiri anayeswali Maghrib kujiunga na imamu katika ´Ishaa


Swali: Kuna mtu ameingia msikitini ilihali ni msafiri na akakuta wanaswali ´ishaa ilihali hajaswali maghrib. Akajiunga nao. Pindi imamu aliposimama katika Rak´ah ya nne akakaa. Je, kitendo chake ni sahihi au hapana?

Jibu: Maoni yaliyo na nguvu ni kwamba kitendo chake ni sahihi. Ukijiunga na imamu ambaye anaswali ´ishaa na wewe hujaswali maghrib, mfuate. Ataposimama katika Rak´ah ya nne, wewe kaa na unuie kutimiza kivyako ambapo utafanya Tashahhud na utoe Tasliym. Baada ya hapo ingia na imamu katika kile kitachokuwa kimebaki katika swalah ya ´ishaa. Haya ndio maoni yenye nguvu.

Baadhi ya wanachuoni wengine wakasema kuwa unatakiwa kwanza kuswali maghrib peke yako au uswali pamoja na wale walio pamoja nawe. Baada ya kumaliza ndio uingie pamoja na imamu katika kile kitachokuwa kimebaki katika swalah ya ´ishaa.

Wanachuoni wengine wakasema unatakiwa kujiunga na imamu kwa nia ya swalah ya ´ishaa. Utapomaliza ndio uswali maghrib.

Haya ndio maoni matatu ya wanachuoni. Lakini maoni yaliyo na nguvu ni yale ya kwanza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa´ ash-Shahriy (01)
  • Imechapishwa: 08/09/2020