Ibn ´Uthaymiyn kuhusu Salafiyyah yenye kusifiwa na yenye kusimangwa

Swali: Tunataka kujua ni nini Salafiyyah. Je, inafaa kwetu kujinasibisha kwayo? Je, inafaa kwetu kumkemea yule asiyejinasibisha kwayo au kumkemea mtu kwa kujiita “Salafiy” na mfano wake?

Jibu: Salafiyyah ni kule kufuata mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Wao ndio watangu walioishi kabla yetu. Kuwafata wao ndio Salafiyyah.

Kuhusu kuchukulia Salafiyyah kama mfumo maalum ambao mtu anajitofautisha na wengine na akawatia upotofuni wale waislamu wengine ijapo watakuwa juu ya haki na kuchukulia Salafiyyah kama mfumo wa kipote, hili ni kinyume na Salafiyyah.

Salaf wote wanalingania katika Uislamu na umoja juu ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawawatii upotofuni wengine wanaokwenda kinyume nao kwa sababu ya kufahamiana kimakosa muda wa kuwa sio katika mambo yanayohusiana na ´Aqiydah. Hata hivyo wanamuona mwengine mwenye ´Aqiydah niyngine kwamba ni mpotofu.

Kuhusu mambo ya kimatendo, ni wenye kuvumiliana sana.

Baadhi ya watu wanaofata Salafiyyah hii leo wanamtia upotofuni kila yule anayekwenda kinyume nao ingawa atakuwa juu ya haki. Baadhi yao wameifanya kuwa ni mfumo wa kipote kama ilivyo mifumo ya vipote vyengine inayojinasibisha na Uislamu. Hili ndio linalopingwa na haliwezi kukubaliwa. Watazame Salaf! Walikuwa wakifanya nini katika mfumo wao na namna walivyokuwa wakivumiliana inapokuja katika mambo ya tofauti ambayo inafaa kufanya Ijtihaad? Walikuwa wakitofautiana mpaka katika mambo makubwa, katika mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na mambo ya kimatendo. Baadhi yao wanakataa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake ilihali wengine wanalithibitisha hilo. Baadhi yao wansema kuwa matendo ndio yatakayopimwa siku ya Qiyaamah ilihali wengine wanasema kuwa mtendaji ndiye atakayepimwa na wengine wakiona kuwa madaftari ya matendo ndio yatakayopimwa. Vivyo hivyo inapokuja katika mambo yanayohusiana na Fiqh wakitofautiana sana kama vile mambo ya ndoa, mirathi, eda, biashara na mengineyo. Licha ya hivyo baadhi hawaonelei wengine kuwa ni wapotofu.

Salafiyyah kama kipote maalum kilicho na sifa zake maalum na kikawatia upotofuni wengine, watu hawa hawana uhusiano wowote na Salafiyyah.

Salafiyyah ni kule kufata mfumo wa Salaf katika ´Aqiydah, maneno, matendo, umoja, kuafikiana, kuoneana huruma na kupendana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa waumini katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kuhisiana kwao ni kama mfano wa mwili mmoja.”

Au alisema:

“Mfano wa waumini katika kupendana kwao, kuhisiana kwao na kuhurumiana kwao ni kama mfano wa mwili mmoja. Kiungo kimoja kikipata maumivu, mwili mzima unapata maumivu kwa homa na kutopata usingizi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=2M_bEhwTrsc
  • Imechapishwa: 17/06/2021