Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kuwaoa wanawake wa kinaswara na wa kiyahudi II

Swali: Ni ipi hukumu ya kuwaoa wanawake wa Ahl-ul-Kitaab; mayahudi na manaswara?

Jibu: Ndugu! Hatuna haki ya kuhukumu isipokuwa kwa yale aliyohukumu Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ

“Leo mmehalalishiwa vilivyo vizuri na chakula cha Ahl-ul-Kitaab ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao na wanawake wenye kujichunga na machafu miongoni mwa waumini wanawake na wanawake wenye kujichunga na machafu miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu… “[1]

Bi maana ni halali. Inajuzu kwa mwanaume kumuoa mwanamke wa kiyahudi na wa kinaswara. Kimsingi mambo ni hivi. Lakini mtu akichelea juu ya nafsi yake au mtoto wake endapo atamuoa mwanamke wa kiyahudi na wa kinaswara atakatazwa kufanya hivo. Sio kwa sababu mwanamke huyo ni haramu. Lakini kwa kuchelea asije kutumbukia katika haramu.

Mtu akiwa ni mwenye dini nyonge na akapendezwa na mwanamke wa kiyahudi na wala hajiamini nafsi yake mwanamke huyo akamvuta katika dini yake, hapo tutamkataza na kumwambia kwamba ni haramu kwake. Kwa sababu kumuoa kwake – na ni halali kwake – ni njia inayopelekea kutumbukia katika haramu. Vivyo hivyo ikiwa atakhofia juu ya watoto wake. Kwa sababu baadhi ya watu ni wenye kufanana na wanaume na si wanaume. Utamuona mwanaume akiwa na kanzu yake na kilemba chake. Lakini uhakika wake ni mwanamke. Akichelea watoto wake kuharibika kupitia mikono ya mwanamke huyu basi asimuoe. Kunasemwa hayohayo juu ya mwanamke wa kinaswara.

Kwa kifupi ni kwamba kimsingi ni kwamba inafaa kwa mwanaume wa Kiislamu kumuoa mwanamke wa kiyahudi au wa kinaswara midhali hachelei madhara. Pindi atapochelea madhara basi atakatazwa. Namna hii kila kitu kinachoruhusiwa (مباح) ikiwa kunakhofiwa madhara kunageuka kuwa haramu. Zinduka na kanuni hii na ichukue, ee mwanafunzi na mtu wa kawaida. Kwa sababu ni kanuni nyepesi sana. Kila kilichoruhusiwa kukikhofiwa juu yake madhara basi kinakuwa haramu.

Muulizaji: Amwache na yale anayofanya kama kunywa pombe na mengineyo?

Ibn ´Uthaymiyn: Ndio. Akimuoa mwanamke wa kiyahudi au wa kinaswara amwache juu ya yale anayoona kuwa ni halali katika dini yake.

[1] 05:05

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (76) http://binothaimeen.net/content/1754
  • Imechapishwa: 22/09/2020