Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kuwalingania waislamu wenye ´Aqiydah mbovu


Swali: Baadhi ya walinganizi wanaona kuanza kulingania na mambo mengine kabla ya ´Aqiydah ambayo wanaona ni mtihani. Tunaomba ubainifu juu ya jambo hili.

Jibu: Ikiwa unawalingania makafiri, basi ni lazima kuanza kwa Tawhiyd. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma Mu´aadh kwenda Yemen na akamwambia:

“Basi iwe jambo la kwanza utakalowalingania kwalo kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah… “

Hata hivyo ikiwa wanaolinganiwa ni waislamu wenye ´Aqiydah mbovu, usikabiliane nao kwa kukemea ´Aqiydah hizi. Kwa sababu wanaona kuwa mambo hayo ni katika dini. Hakikisha unawahimiza katika swalah, kutoa swadaqah, kufunga na kuhiji mpaka pale watakapozowea na kuhisi utulivu kwako. Kisha baada ya hapo wabainishie kuwa ´Aqiydah yao ni mbovu.

Kwa hiyo kuna tofauti kati ya wale wanaolinganiwa. Ukianza kumlingania kafiri kwa Tawhiyd na akakataa, yeye ni kafiri tokea mwanzo. Lakini huyu wa pili ni muislamu na amekosea katika Bid´ah yake aliyozua na akadhani kuwa ni haki. Kwa ajili hiyo usikabiliane naye kwa makaripio. Kuna khatari akakimbia na asikubali kutoka kwako chochote. Mlinganie katika mambo ambayo hakuna tofauti kama vile swalah, swadaqah, kufunga na kuhiji. Baada ya hapo, wakishajisi utulivu na wakaona kuwa yale unayosema ni haki, basi inakuwa ni wepesi sana kuingia ndani ya maudhui na kuwabainishia Bid´ah na kwamba ni haramu na ni wajibu kuziepuka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (56 B)
  • Imechapishwa: 10/06/2021