Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kutaja kosa la mtu ambaye anatahadharishwa

Swali: Tunakuuliza swali hili juu ya mtu ambaye ni katika wanazuoni na matendo na amesifiwa kwa kheri na juhudi yake katika Da´wah, naye si mwengine ni muheshimiwa Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin ´Abdil-Khaaliq (Hafidhwahu Allaah). Tunaomba kusikia yale unayoyajua juu ya Shaykh huyu.

Jibu: Sio katika mfumo wetu katika vikao hivi kuwazungumzia watu kwa majina yao. Lakini tunachosema ni kwamba, kila mtu ambaye ana cheo kitukufu katika Ummah wa kiislamu, kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake, hapana shaka kwamba anasifiwa kwa yale matendo mema aliyoyafanya.

Pasi na kujali mtu atakuwa mjuzi na mchaji kiasi gani, hasalimiki na makosa kutokana na ujinga, ughafilikaji na sababu nyenginezo. Lakini kama alivosema Ibn Rajab (Rahimahu Allaah), mwanzoni mwa kitabu chake “al-Qawaa´id”, mwadilifu ni yule anayeficha makosa madogo yanayofanywa na mtu ambaye kupatia kwake ndio kwingi zaidi. Hakuna mtu yeyote anayeyavalia njuga makosa na akayafumbia macho mazuri isipokuwa anakuwa ni mwenye kujifananisha na wanawake. Ukimtendea wema mwanamke mwaka mzima kisha siku moja akaona kitu kibaya kutoka kwako, husema:

“Sijapatapo kuona kitu kizuri hata siku moja.”

Hakuna mwanamme yeyote anayependa kuwa kama wanawake ambapo anashikilia kosa moja na akasahau mazuri mengi.

Kanuni hii, ambayo ni kutozungumzia watu kwa kuwalenga katika darsa na vikao vyetu, ndio kanuni ambayo mimi natembelea juu yake. Namuomba Allaah anithibitishe juu yake. Kwa sababu kuwazungumzia watu kwa kuwalenga kunaweza kupelekea katika makundi na ushabiki. Ni wajibu kuyatunza mambo kwa wasifu na si kupitia watu. Hivyo mtu akasema ambaye anafanya kadhaa anastahiki kadhaa, pasi na kujali ni kheri au shari.

Lakini pindi tunapotaka kumthamini mtu, basi ni lazima kuyatazama mazuri na mabaya. Kufanya hivo ndio uadilifu.

Wakati tunapotahadharisha kosa la mtu, tunatakiwa kutaja kosa peke yake. Kwa sababu inahusiana na matahadharisho. Nafasi ya matahadharisho sio hekima kutaja yale mazuri. Ukitaja yale mazuri, basi wasikilizaji wanakuwa wenye kuchanganyikiwa. Kila kitu kinategemea na hali yenyewe.

Ambaye anataka kumthamini mtu, basi ni lazima kwake kutaja mazuri na mabaya yake kukiwa kuna haja ya kufanya hivo. Vinginevyo vizuri ni kutotaja mabaya ya waislamu.

Kuhusu ambaye anataka kutahadharisha kosa fulani, huyu ataje kosa. Akiweza kutomtaja mwenye kosa hilo, ndio vizuri pia. Kwa sababu lengo ni kuwaongoza viumbe.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (67 A)
  • Imechapishwa: 18/07/2021