Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kuomba kwa jaha ya Mtume (´alayhis-Salaam)

Swali: Je, inajuzu kufanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Kufanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo lisilojuzu kwa mujibu wa maoni yenye nguvu ya wanachuoni. Kwa hivyo ni haramu kufanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haifai kwa mtu kusema: “Ee Allaah! Mimi nakuomba kitu fulani kwa jaha ya Mtume.” Hilo ni kwa sababu njia haiwi njia isipokuwa ikiwa iko na athari katika kufikia lile lengo. Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa nisba ya muombaji haina athari katika kufikia lengo. Ikiwa haina athari yoyote basi haiwi sababu sahihi. Allaah (´Azza wa Jall) haombwi isipokuwa kwa kile kilicho na sababu sahihi kilicho na athari katika kufikia lengo. Jaha ya Mtume ni katika mambo ambayo ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Ni katika mambo ambayo yatakuwa ni sifa kwake peke yake. Kuhusu sisi hatutonufaika kwayo. Kitachotunufaisha ni kumuamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumpenda. Kuna wepesi wa aina gani kwa yule mwombaji endapo atasema: “Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kitu fulani kwa kukuamini na kwa kumuamini Mtume wake” badala ya yeye kusema: “Ee Allaah! Mimi nakuomba kwa jaha ya Mtume”.

Miongoni mwa neema za Allaah (´Azza wa Jall) na huruma Yake ni kwamba hafungi mlango wowote wa madhara isipokuwa mbele ya mtu huyo kuna milango mingi iliyoruhusiwa. Himdi zote zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/348)
  • Imechapishwa: 10/07/2017