Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kunyoa nywele za miguuni na mikononi

Swali: Ni ipi hukumu ya kuondosha nywele za miguuni na mikononi?

Jibu: Zikiwa nyingi basi hakuna ubaya kuziondosha. Kwa kuwa zinaleta muonekano mbaya. Ikiwa ni za kawaida basi kuna wanachuoni wenye kuoenelea kuwa kuziondosha ni katika kuyabadilisha maumbile ya Allaah (´Azza wa Jall). Wengine wakasema kuwa ni miongoni mwa mambo yenye kufaa kwa kuwa ni katika mambo ambayo Allaah ameyanyamazia. Hoja yao ni pale Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Kuhusu yale Allaah aliyoyanyamazia ni msamaha.”

Bi maana sio lazima wala haramu kwenu. Watu hawa wamesema kuwa Shari´ah imegawanyika katika sehemu tatu:

Ya kwanza: Kuna mambo Shari´ah imefahamisha juu ya uharamu wake kuyaondosha.

Ya pili: Kuna mambo Shari´ah imefahamisha juu ya kutakikana kwake kuondoshwa.

Ya nne: Mambo ambayo Shari´ah imeyanyamazia.

Kuna mambo ambayo Shari´ah imefahamisha juuu ya uharamu wake kuyaondosha. Kama mfano wa ndevu kwa mwanaume, kunyoa nyusi kwa mwanaume na mwanamke.

Kuna mambo Shari´ah imefahamisha juu ya kutakikana kwake kuondoshwa. Kama mfano wa nywele za kwapani, nywele za sehemu za siri na masharubu kwa mwanaume.

Kuna mengine ambayo Shari´ah imeyanyamazia. Hayo ni msamaha. Kwa sababu lau ingelikuwa ni miongoni mwa mambo asiyotaka Allaah kuwepo kwake, basi angeliamrisha kubaki kwake, kama ambavyo lau ingelikuwa ni miongoni mwa mambo anayotaka Allaah yabaki, basi angeliamrisha zibaki. Midhali Allaah ameyanyamazia basi yanarudi vile anavyotaka mtu; akitaka kuziondosha atafanya hivo na akitaka kuzibakiza atafanya hivo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/134)
  • Imechapishwa: 30/06/2017