Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kumshuhudilia yeyote Pepo au Moto


Swali: Miongoni mwa ´Aqiydah zilizothibiti kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba hawamkatii yeyote Pepo wala Moto isipokuwa yule aliyeshuhudiwa na Allaah na Mtume wake. Je, katika haya wanaingia myahudi na mnaswara pindi wanapokufa basi hatutakiwi kusema kuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni au mambo yanatofautiana?

Jibu: Mosi tunatakiwa kutambua kuwa kushuhudia Pepo au Moto haiwi isipokuwa kwa yule aliyeshuhudiwa na Allaah na Mtume wake. Kuna ushuhuda aina mbili:

Ya kwanza: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumshuhudia mtu kwa dhati yake. Huyu na sisi vilevile tunatakiwa kumshuhudilia. Ni mamoja inahusiana na Pepo au Moto. Vilevile endapo Allaah atamshuhudilia mtu kwa dhati yake ya kwamba yuko Pepo au Motoni basi na sisi tutatakiwa kufanya vivyo hivyo. Mfano wa ambaye Allaah amemshuhudilia kwa dhati yake kwamba yuko Motoni ni Abu Lahab ambaye ni ami yake Mtume Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ  سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِّن مَّسَدٍ

“Imeteketea mikono miwili ya Abu Lahab na ameteketea. Haikumfaa kitu mali yake na wala yale aliyoyachuma. Ataingia na kuungua moto wenye mwako na mke wake mbebaji kuni za moto. Shingoni mwake kamba ya mtende iliyosokotwa madhubuti.” (111:01-05)

Mfano wa ambaye Allaah amemshuhudilia Pepo ni Abu Bakr kwa mujibu wa moja ya maoni juu ya maneno Yake (Ta´ala):

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ

“Ataepushwa nao yule mwenye taqwa kabisa, ambaye anatoa mali yake kujitakasa na hali hakuna mmoja yeyote aliyemfanyia fadhila yoyote ili amlipe, isipokuwa kutaka Uso wa Mola wake Aliyetukuka. Bila shaka atakuja kuridhika.” (92:17-21)

Wafasiri wengi wa Qur-aan wamesema kuwa mlengwa ni Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh). Tafsiri hii ikiwa ni ya sawa na kwamba kweli inamuhusu Abu Bakr kwa dhati yake – lakini kinachozingatiwa ni kule kuenea kwa tamko – vinginevyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemshuhudilia Pepo na akamshuhudilia ya kwamba ni mkweli mno (as-Swiddiyq). Hapo ilikuwa pindi Mtume Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan walipopanda juu ya mlima wa Uhud baada ya tukio fulani. Mnjua mlima ulifanya nini? Ulitikisa. Hapa ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliuambia mlima:

“Tulia. Hakika juu yako yuko Mtume, as-Swiddiyq na mashahidi wawili.”

Hawa ambao wameshuhudiliwa na Allaah na Mtume wake na sisi tunatakiwa kuwashuhudilia kwa dhati zao.

Ya pili: Ushuhuda wa aina na si kwa dhati. Tunashuhudia ya kwamba kila muumini na mwenye kumcha Allaah kwamba yuko Pepo na wakati huohuo tunatakiwa kushuhudia ya kwamba kila kafiri yuko Motoni. Ama kuhusu mtu kwa dhati yake hatutakiwi kufanya hivo.

Lakini yule mwenye kufa katika hali ya kudhihirisha ukafiri na kuupiga vita Uislamu, ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba Uislamu unakaribia kuyakinisha ya kwamba ni katika watu wa Motoni. Lakini iwapo mtu asingelikuwa anachelea asije kuadhibiwa kwa kuteleza kwa ulimi basi angelimshuhudilia mtu wa sampuli hii. Lakini hata hivyo sawa mtu ashuhudie au asishuhudie; ikiwa mtu ni wa Motoni atabaki kuwa wa Motoni hata kama utashuhudia kuwa alikuwa mwema, na kama si katika watu wa Motoni hata kama utashuhudia mara elfumoja kwamba ni katika watu wa Motoni hatokuwa katika watu wa Motoni na hakuna kitachopelekea katika hilo. Lakini hapana shaka yoyote dhana iliyo na nguvu zaidi – kama haifikii yakini kabisa – kwa yule mwenye kufa katika ukafiri, hali ya kumpiga vita Allaah na Mtume wake ya kwamba yuko Motoni. Lakini mtu anachelea tu asije kuteleza ulimi juu ya ushuhuda huu. Kwa sababu Allaah amesema:

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hatamki yeyote neno isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha [kuandika].” (50:18)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (31) http://binothaimeen.net/content/699
  • Imechapishwa: 03/11/2017