Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kukunuti katika swalah ya Fajr

Swali: Kuleta du´aa ya Witr katika Rak´ah ya mwisho ya swalah ya Fajr ni jambo limewekwa katika Shari´ah?

Jibu: Du´aa ya Witr ijulikanayo ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayahi wa sallam) alimfunza al-Hasan bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) isemayo:

اللهم اهدني فيمن هديت, وعافني فيمن عافيت, وتولني فيمن توليت, وبارك لي فيما أعطيت, وقني شر ما قضيت, فإنك تقضي ولا يقضى عليك, وإنه لا يذلّ من واليتَ, ولا يعزّ من عاديت, تباركت ربنا وتعاليت، لا منجا منك إلا إليك

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na wale Uliowaongoza, uniafu pamoja na wale Uliowaafu, Uniangalie pamoja na wale Unaowaangalia, Unibariki katika kile Ulichotoa na Unilinde kutokamana na shari kwa yale Uliyohukumu. Kwani hakika Wewe ndiye mwenye kuhukumu na wala Huhukumiwi. Hakika hatwezeki yule Uliyemfanya mpenzi na wala hapati nguvu yule Uliyemfanya adui. Umebarikika na Umetukuka Mola wetu. Hakuna mahali pa kuokoka kutokamana na Wewe isipokuwa Kwako.”

imethibiti katika Witr peke yake. Haikuthibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayahi wa sallam) alikuwa akileta Qunuut katika Fajr wala katika swalah nyingine. Kukunuti kwa du´aa hii katika Fajr ni jambo lisilokuwa na msingi katika Sunnah.

Kuhusu kukunuti katika Fajr kwa du´aa nyingine mbali na du´aa hii ni jambo wanachuoni wametofautiana katika maoni mawili. Maoni ya sawa ni kwamba hakutakiwi kukunutiwa katika Fajr isipokuwa kwa kuwepo sababu inayohusiana na waislamu wote kwa jumla. Kwa mfano waislamu wafikwe na maradhi ya mlipuko, mbali na tauni, basi wanatakiwa kuleta Qunuut katika swalah za faradhi ili Allaah aweze kuwaondoshea janga hilo.

Pamoja na haya iwapo kuna imamu anayeleta Qunuut katika swalah ya Fajr basi anatakiwa kufuatwa katika Qunuut hiyo na maamuma waitikie “Aamiyn” juu ya du´aa yake. Hivyo ndivyo alivyosema Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Kwa sababu hili ni kwa minajili ya kuwafanya waislamu kuwa na umoja.

Ama kutokea uadui na bughudha juu ya Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayahi wa sallam) katika mfano wa tofauti kama hizi ambazo Ijtihaad inakubalika ni jambo lisilotakikana. Bali kinachotakikana kwa wanafunzi ni vifua vyao viwe vipana vyenye kuweza kupokea tofauti kati yao na ndugu zao. Hili ni khaswa pale ambapo wataelewa kutoka kwa ndugu zao ya kwamba wana malengo mazuri na salama na kwamba hakuna wanacholenga isipokuwa haki na masuala hayo yakawa ni yenye kuingia katika mlango wa Ijtihaad. Ijtihaad yako si yenye haki zaidi ya kuwa ya sawa kuliko Ijtihaad ya yule anayetofautiana na maoni yako. Haya yanahusiana na Ijtihaad na hakuna dalili ya wazi. Ni vipi utakemea Ijtihaad yake na wala hukemei Ijtihaad yako mwenyewe? Haya si mengine isipokuwa ni jeuri na uadui katika hukumu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/129-130)
  • Imechapishwa: 17/06/2017