Ibn ´Uthaymiyn kuhusu idadi ya Rak´ah za Tarawiyh

Swali: Je, Tarawiyh ni katika kisimamo? Ni ipi Sunnah inapokuja katika kisimamo cha Ramadhaan? Ni idadi zipi ambazo ni bora kuswali?

Jibu: Tarawiyh ni katika kisimamo [cha usiku].

Sunnah inapokuja katika kisimamo cha Ramadhaan ni kuitekeleza mkusanyiko msikitini kutokana na kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati aliposimama na Maswahabah wake nyusiku tatu kisha akasitisha kufanya hivo kwa kuchelea isije kufaradhishwa kwao.

Lililo bora ni mtu kukomeka na ile idadi aliyoswali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa ni vipi ilikuwa swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan ambapo akajibu:

“Alikuwa hazidishi Ramadhaan wala mwezi mwingine juu ya Rak´ah kumi na moja.”

Vilevile imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba aliswali Rak´ah kumi na tatu. Kwa hivyo idadi inakuwa ima Rak´ah kumi na moja au kumi na tatu.

Hata hivyo hakuna neno endapo mtu atazidisha juu ya idadi hii. Lakini kilicho muhimu ni kuwa na utulivu na kutofanya haraka ili waswaliji walioko nyuma ya imamu waweze kuzikamilisha swalah zao. Imamu ni mwenye kuaminiwa juu yao. Kwa hivyo ni wajibu kwake kuwajali na asiwanyime utulivu ambao utawafanya waweze kufanya kilicho na ukamilifu zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/189-190)
  • Imechapishwa: 17/06/2017