Ibn ´Uthaymiyn kuhusu duka la vitabu lililo na vitabu vya Ahl-ul-Bid´ah

Swali hili ni muhimu. Manufaa na madhara ya maduka ya vitabu inatokana na mambo mawili:

1 – Vitabu. Ni vitabu gani? Je, ni vitabu vya Salafiyyah vilivyojengeka juu ya madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah? Au ni vitabu vya kifikra zilizopinda? Ikiwa ni hilo la kwanza, basi ni neema ilioje ya maduka ya vitabu. Na ikiwa ni hilo la pili, basi ni lazima kurekebisha.

2 – Wamiliki. Wao ni kina nani? Ni upi mfumo wao? Ni vipi ´ibaadah na tabia zao? Ni lazima wamiliki iwe miongoni mwa wale watu ambao inaaminiwa elimu, dini, tabia na mfumo wao.

Kwa sababu maduka ya vitabu hivi ndio makimbilio ya vijana. Ujana ni kama unga mikononi mwa mwokaji mikate. Unakuwa vile unavokandwa. Akiongozwa na watu wema ambao watamshauri katika yale yaliyo na munufaa katika dunia na Aakhirah, basi atanufaika kwa maduka ya vitabu hivi. Watakuwa ni vyanzo vya kheri kwa vijana. Ikiwa wamiliki wanazo fikra zilizopinda na ambazi si salama, basi hapo ndipo kwenye madhara. Ima wabadilishwe wamiliki au maduka haya ya vitabu yafungwe. Uislamu umejengeka katika kuyafikia manufaa yaliyo safi kabisa au yaliyo na uzito zaidi na kujiepusha na madhara yaliyo safi kabisa au yaliyo na uzito zaidi. Na ikiwa jambo linalo manufaa na madhara, basi kutatangulizwa mbele kile kilicho na nguvu zaidi katika mawili hayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا

”Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na manufaa [fulani] kwa watu; na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.”[1]

Ndio maana yakaharamishwa. Ikiwa manufaa ndio makubwa zaidi, basi  yatatendewa kazi na hivyo madhara yataingia ndani ya manufaa. Kama ambavo kanuni hii inatumika juu ya matendo, inatumika vilevile juu ya mtendaji mwenyewe. Je, kila mwenye kufanya matendo mema hufanya mema peke yake? Hapana. Wanafanya matendo mazuri na mabaya. Hata hivyo miongoni mwa watu wako ambao matendo yao mema ndio mengi zaidi na wako watu ambao matendo yao mabaya ndio mengi zaidi. Kwa ajili hiyo haijuzu kuwaangalia waislamu kwa upande wa shari peke yake. Bali inatakiwa iwe kwa pande zote mbili ili tuweze kupima na kulinganisha. Baada ya hapo mtu atendee kazi kile chenye kudhihiri.

Ikiwa maduka ya vitabu yanasimamiwa na watu wema ambao ni wanazuoni na watu waaminifu na wana mfumo na tabia njema, basi ni mradi bora kabisa kwa sharti vitabu viwe vizuri. Ni jambo linalotambulika kwamba ikiwa wamiliki ni wema, basi wayatalinda kutokamana na vitabu vilivyopinda kifikra, ki-´Aqiydah au kimfumo.

[1] 02:219

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (173 A) Tarehe: 1418-08-04/1997-12-04
  • Imechapishwa: 14/07/2021